RC aonya NGOs, vigogo wa wilaya ya Ngorongoro - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » RC aonya NGOs, vigogo wa wilaya ya Ngorongoro

RC aonya NGOs, vigogo wa wilaya ya Ngorongoro

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Monday, June 3, 2013 | 11:50 AM

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo


MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali (NGOs) na Baraza la wafugaji wilayani Ngorongoro wameonywa kuacha kunogewa na fedha haramu wanazozipata, zinazowatuma kuchochea vurugu baina ya wananchi, mamlaka ya hifadhi na serikali.

Mbali ya NGOs, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wanaotaka kuwania ubunge wa Jimbo la Ngorongoro mwaka 2015 na mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Saning’o ole Telele na Mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Mathew ole Timani na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Ngorisa, wametakiwa kuacha kutumia mgogoro huo kujitafutia umaarufu.

Onyo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara baina yake wananchi na viongozi wa kata ya Enduleni wilayani Ngorongoro ili kutatua mgogoro kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na wananchi walio ndani ya hifadhi hiyo.


Mulongo alisema mashirika hayo na wanasiasa hao, wamekuwa wakiwapotosha wananchi kuwa serikali imewatelekeza.

Alisema serikali ina mpango wa kuiingiza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, iwe chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wananchi hao watalazimika kufukuzwa.

Alisema kwa muda mrefu, asasi hizo na wanasiasa wamekuwa wakichochea vurugu kwa kutoa matamshi yasiyo ya kiungwana, ikiwemo kuhakikisha wanafanikiwa malengo yao ya matumizi ya fedha walizopewa na wafadhili wao pasipo kuangalia athari za matamshi yao kwa nchi.

Mulongo alisema hivi karibuni mashirika, asasi na baraza hilo la wafugaji, wamefikia hatua ambayo si nzuri ya kuwasemea wananchi hadi kutoa matamko ambayo ni hatari.

Pia, walitoa masharti kuwa iwapo serikali itaendelea kushikilia uamuzi wake wa kuwaondoa wananchi hao katika maeneo yao, watashirikiana nao kufunga mageti ya kuingilia watalii ndani ya hifadhi hiyo ili kuzuia shughuli za utalii.

Hata hivyo, alilinyoshea kidole baraza la wafugaji Ngorongoro kwa kuwawezesha chini kwa chini wananchi na baadhi ya viongozi wa serikali na madiwani kwa mambo mbalimbali ya kichochezi, ikiwemo gharama za kwenda mikoa ya Dodoma,Dar es Salaam na hata mjini Arusha kwa ajili ya kuendeleza vurugu hizo.

Akiwazungumzia wanasiasa hao, alisema wamekuwa wakichuana katika kampeni zao zisizo rasmi kwa kutumia mgogoro huo usio na mantiki, kujitafutia umaarufu.

Alitaka watumie njia nyingine ya kutafuta umaarufu huo badala ya kuendelea kuwagawa wananchi na hifadhi na serikali yao.

By John Mhala, Arusha
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger