Wanaotumia gesi Mtwara kuvuruga nchi washughulikiwe - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » Wanaotumia gesi Mtwara kuvuruga nchi washughulikiwe

Wanaotumia gesi Mtwara kuvuruga nchi washughulikiwe

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Sunday, May 26, 2013 | 8:44 PM


 
    

SUALA la vurugu za Mtwara zinazoelezwa kuchangiwa na kupinga bomba la gesi kujengwa ili kusafirisha rasilimali hiyo kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam, zilizotokea juzi, zinaashiria wazi kuwa, wapo watu wenye kauli na ushawishi mkubwa nyuma ya jambo hilo.


Nasema hivyo kwa kuwa, haiingii akilini kwamba, suala lenye manufaa kwa Taifa zima kwa kuanzia na Wana Mtwara wenyewe, linaweza kupingwa kwa mtindo huo wa vurugu, kusababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali kama vile hakukuwa na nia nyingine mbadala ya kufikisha ujumbe.

Nashawishika kuamini kuwa, hili halifanywi na Wana-Mtwara bali wapo baadhi ya watu kama walivyosema viongozi wa kitaifa kwamba, wanawatumia watu waliozoea fujo, wasiojua thamani ya amani ya nchi, wanawatumia wananchi wachache kuharibu amani na nia njema ya serikali kuinua kiuchumi, mikoa ya pembezoni, yenye maendeleo duni.

Hakuna anayepinga ukweli kwamba, mkoa wa Mtwara na mikoa kadhaa ya kusini, ni miongoni mwa maeneo yenye maendeleo finyu, wakati tukiilinganisha na mikoa mingine iliyoinuka kiasi kiuchumi, tuzingatie utamaduni na historia pia, suala hili limezungumzwa sana na viongozi wa nchi sambamba na kueleza mikakati ya namna ya kuikomboa mikoa hiyo iliyoko nyuma kiuchumi.

Serikali imeeleza mengi kuhusu mikakati hiyo wala sina haja kuieleza hapa, lakini ikumbukwe kuwa, mara baada ya vurugu za gesi kama zilizotokea juzi, kutokea Mtwara mwishoni mwa mwaka jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alikwenda mkoani humo na kueleza namna gesi hiyo itakavyowanufaisha wananchi wa huko.

Pamoja na mambo mengine, Pinda aliwaelimisha jinsi viwanda vya mbolea vitokanavyo na gesi ghafi vitakavyojengwa mkoani humo na kutoa ajira kwa wakazi wa hapo hasa vijana, namna umeme utakaozalishwa utakavyoingizwa kwenye gridi ya Taifa na kumnufaisha kila Mtanzania.

Ufafanuzi huu pia uliwahi kutolewa kupitia vyombo vya habari na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, mara baada ya vurugu za mwaka jana.

Kama hiyo haitoshi, juzi Rais Jakaya Kikwete, akiwa mkoani Dodoma alitoa kauli kuhusu suala hilo mara baada ya vurugu kutokea, alisema watu wanaotumia suala hilo kwa maslahi yao binafsi, hawatavumilika, watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Kauli ya Rais Kikwete na viongozi wengine, inaashiria wazi suala hili limefika kikomo, sijui kama wakazi wa Mtwara wanakumbuka namna suala la usafiri lilivyokuwa kero mkoani mwao, wanakumbuka jinsi abiria walivyokaa njiani wiki moja za zaidi katika eneo la kufika kwa saa sita, kutokana na ubovu wa miundombinu?
Leo yamejengwa madaraja, barabara za lami, mikakati ya kuinua zao la korosho inavyopamba moto, vyuo vya elimu ya juu na ya kawaida vilivyojengwa, vituo vya afya, shule binafsi na za serikali, maeneo ya uwekezaji na sasa ujio wa gesi asilia ambayo kwa hakika lazima iwanufaishe wakazi wa huko kama ilivyoelezwa.

Mambo hayo ndio yananishawishi kuunga mkono kauli za viongozi wa Kitaifa kuwa, vurugu hizi zina watu wenye sauti katika jamii nyuma yake, wapo watu kama si wanasiasa wanaotafuta umaarufu kwa damu za Watanzania, basi niwaite maharamia wanaotaka kuiteka meli (Tanzania) na kuizamisha baharini ili sote tufe. Prof. Muhongo ameeleza namna wizara ilivyotoa kijitabu na machapisho mbalimbali kuelimisha na kufafanua faida za gesi ya Mtwara kwa taifa na mkoa husika.

Nadhani ni wakati muafaka ikiwa wachochezi hawajapata muda wa kuyasoma machapisho hayo, basi wafanye hivyo ili kupima katika mizani na kutumia utashi waliopewa na Mungu, lipi bora kati ya vurugu na amani.

Nadhani njia sahihi ni kupinga suala hili kwa hoja ama kwenda mahakamani na si kuchochea vurugu. Niliwahi kusema kupitia wazo langu kwamba, vita ikitokea Tanzania, kwa namna tulivyooleana, kuchanganyika kimakabila na dini, hakika hakuna atakayesalia. Ndio maana nina ujasiri kukemea kila mwenye nia mbaya juu ya amani yetu.

Waandishi wa habari na vyombo vyetu tuepuke kuandika habari za kuchochea vurugu badala yake, tujikite zaidi kwenye kutoa elimu, tuwaeleze watu kuhusu ubora wa mradi huo unaogharimu Dola za Marekani mil 1,225.3 uliozinduliwa Novemba mwaka jana na Rais Kikwete na kuwafichua wenye nia mbaya na maendeleo ya nchi.

Ni vema serikali isisitishe ujenzi wa bomba hilo la urefu wa kilometa 532 na kipenyo cha nchi 36 lenye uwezo wa kusafirisha futi za ujazo za gesi milioni 784 kwa siku, kwa maslahi ya Taifa.

Niombe pia isiishie kutoa matamko na misimamo bali ishirikiane na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola, kuhakikisha kuwa, kila anayehusika na uvunjifu huu wa amani, anashughulikiwa ipasavyo.
By Gloria Tesha
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger