SERIKALI ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro imelaani vitendo vilivyofanywa na watu wanodaiwa kuwa ni wafuasi wa CHADEMA kufanya vurugu, kuchoma moto tairi na kuweka mawe barabarani katika kijiji cha Ruaha wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Wafuasi hao walifanya vurugu kupinga kuteuliwa kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa nafasi hiyo uliofanyika Mei 5 mwaka huu.
Akitoa tamko kwa vyombo vya habari wilayani Kilosa Mkuu wa wilaya hiyo, Elias Tarimo alisema watu watano wanashikiliwa na Polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuhusika na uchochezi wa vurugu hizo baada mgombea wa uchaguzi huo kutoka Chadema kuenguliwa kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya sifa ya kugombea nafasi ya uenyekiti Machi 2 mwaka huu.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa Serikali inapinga na kulaani vikali kitendo hicho cha baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kuufanyia vurugu uongozi halali wa kijiji hicho sambamba na kufunga barabara hiyo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya huyo kitendo hicho ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na ni uhalifu
usiovumilika na ni ukiukwaji wa misingi ya demokrasia, utawala bora na utawala wa haki za binadamu.
Aidha alisema, uongozi wa wilaya chini ya Kamati ya Ulinzi ya Wilaya inawataka watu wote wanaochochea na kufanya vurugu eneo la Ruaha waache mara moja vitendo hivyo viovu kwani wanavunja sheria.
Alisema kuwa Serikali inasisitiza kuwa wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani Ruaha watachukuliwa hatua kali za kisheria na kwamba Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayevunja amani ya eneo hilo wilayani Kilosa kwa kisingizio chochote na kuwataka wananchi wa Ruaha kudumisha amani na upendo na mshikamano.
Hata hivyo alisema kuwa majina ya watu walikamatwa hayataweza kutajwa kufuatia uchunguzi unaoendelea kufanywa katika eneo hilo na kwamba uchunguzi ukikamilika watuhumiwa hao watajulikana.
Vurugu hizo zilitokea Mei 9 mwaka huu siku chache baada ya uchaguzi huo kuisha na kwamba matokeo ya uchaguzi huo yalionesha kuwa mgombea pekee wa CCM kwenye uchaguzi huo alipita baada ya mgombea wa Chadema kuenguliwa na Kamati ya Rufaa ya Wilaya kwa kuwa alishindwa kukidhi vigezo vya kupata sifa za kugombea nafasi hiyo.
Aidha alisema kuwa siku ya tukio Mwenyekiti mteule wa CCM wakati akienda kukabidhiwa ofisi ndipo wananchi wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema walivamia sehemu walipokuwa wamekutana kwa makabidhiano eneo la Shule ya Msingi Ruaha B kwenye darasa na kuanza kuwafanyia fujo.
Alisema polisi waliwahi kufika kwenye eneo la tukio na kuzima vurugu hizo na kwamba hata hivyo wafuasi hao waliendelea kufanya vurugu katika maeneo mengine ya mitaa kwa kufanya maandamano na kuziba barabara kuu ya Mikumi hadi Ifakara, kuchoma matairi barabarani na kuvunja nyumba ya Rashidi Kisaluni ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kijiji aliyeteuliwa na kuharibu vitu vyote vya ndani ambavyo thamani yake bado haijafahamika.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !