SERIKALI imelaani vikali vurugu zilizotokea Mtwara juzi na imeapa kuwasaka waasisi wa vurugu hizo ndani na nje ya Mtwara na ndani na nje ya nchi ili waliohusika kupanga, kushawishi, kuandaa na kutekeleza vurugu hizo wafikishwe kwenye mkono wa sheria. Hadi jana, watu 91 walikuwa wamekamatwa wakituhumiwa kufanya mikusanyiko isiyo halali na uharibifu wa mali na miundombinu.
Aidha Serikali imeapa kuwa damu ya askari wanne wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliokufa katika ajali wakati wakitokea Nachingwea kwenda Mtwara kudhibiti vurugu hizo haitamwagika bure. Hayo yamo katika kauli ya Serikali iliyotolewa bungeni mjini hapa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusiana na vurugu hizo zilizotokea Mtwara juzi.
Akiwasilisha kauli hiyo ya awali ya Serikali bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 49 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili 2013, Dk Nchimbi alisema watu waliohusika na vurugu hizo hawataukwepa mkono wa sheria popote pale walipo. Alisema Mei 22, mwaka huu zilitokea vurugu kubwa katika Manispaa ya Mtwara na viunga vyake kiini kikiwa ni madai ya baadhi ya wananchi wa Mtwara kupinga usafirishaji wa rasilimali ya gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Alisema katika kutimiza hilo, Mei 15, mwaka huu, kikundi cha watu ambao hawakufahamika walisambaza vipeperushi vyenye lengo la kuhimiza wakazi wa Mtwara kuwa siku ya Ijumaa Mei 17, saa 3 asubuhi wasikilize hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ikisomwa bungeni ili kujua mustakabali wa gesi kutosafirishwa kutoka Mtwara.
“Vipeperushi hivyo vilihimiza huduma zote za kijamii zisimamishwe siku hiyo. Pamoja na vipeperushi hivyo, tarehe 17, Mei, 2013 huduma zote za kijamii kama vile usafiri wa magari (daladala), pikipiki (bodaboda) na baadhi ya bajaj zilifanya kazi wakati huduma za maduka na migahawa zilifungwa.
“Hata hivyo hotuba hiyo haikusomwa bungeni siku hiyo. Kikundi hicho kiliendelea kuhamasisha kwa kutumia mitandao ya simu na karatasi za vipeperushi na kuwahimiza wananchi wasikilize hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini pindi itakaposomwa,” alisema Waziri Nchimbi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, matukio hayo yaliendelea tena Mei 22, mwaka huu ambapo majira ya saa 4 asubuhi makundi ya vijana waliokuwa wanasikiliza hotuba hiyo waliokuwa maeneo ya Sokoni, Magomeni na Mkanaredi walipanga mawe makubwa, magogo na kuchoma moto matairi barabarani.
Alisema hali hiyo iliendelea kusambaa maeneo mengine ya mji kama vile Chuno, Chikongola, Mikindani na kutoka nje ya mji hadi Mpapura umbali wa kilomita 40 kutoka Mtwara Mjini na kwamba Jeshi la Polisi lilikabiliana na hali hiyo ya vurugu kwa kurudisha katika hali ya kawaida ya usalama na kuondosha magogo na mawe yaliyokuwa barabarani.
Akizungumzia athari za vurugu hizo, Dk Nchimbi alisema ofisi ya Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtwara Mjini, Hasnain Mohamed Murji iliyopo Mikindani imeharibiwa na kuibiwa vitu mbalimbali, ofisi ya Mahakama ya Mwanzo ya Mitengo imechomwa na kuteketea na nyaraka za ofisi.
Madhara mengine ni kuchomwa moto kwa ofisi ya CCM ya Kata ya Chikongola, kuchomwa moto kwa nyumba binafsi ya Ofisa Mtendaji Kata ya Magomeni, kuchomwa moto kwa nyumba ya Mwandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) wa Mtwara, Kassimu Mikongoro, kuibiwa na kuvunjwa kwa nyumba za askari wanne na kuibiwa vitu mbalimbali katika Ofisi ya Kata ya Chikongola.
Alisema mpaka sasa mtu mmoja Karim Shaibu amefariki dunia katika vurugu hizo na kwamba askari wawili walijeruhiwa kwa bomu la kishindo. Waziri Nchimbi alisema pamoja na kukamatwa watuhumiwa hao 91, alisema vurugu hizo zimedhibitiwa na operesheni ya kuhakikisha hali ya usalama inarejea inaendelea
.
Vifo vya wanajeshi Akizungumzia sababu za kufa kwa wanajeshi wa JWTZ, Dk Nchimbi alisema kutokana na kuzorota kwa usalama, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa mujibu wa sheria aliomba kwa Waziri wa Ulinzi kuongezewa nguvu kulinda raia wasio na hatia na mali zao na Waziri alikubali na kuelekeza JWTZ waende mara moja.
Vifo vya wanajeshi Akizungumzia sababu za kufa kwa wanajeshi wa JWTZ, Dk Nchimbi alisema kutokana na kuzorota kwa usalama, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa mujibu wa sheria aliomba kwa Waziri wa Ulinzi kuongezewa nguvu kulinda raia wasio na hatia na mali zao na Waziri alikubali na kuelekeza JWTZ waende mara moja.
“Katika kutekeleza agizo hilo askari 32 wa Jeshi la Wananchi walianza safari kutoka Nachingwea kwenda Mtwara. Walipokuwa njiani katika eneo la Kilimani Hewa gari lao lilipata ajali ambapo askari wanne walifariki dunia na 20 kujeruhiwa.
“Askari hawa wamefariki na kujeruhiwa wakati wakiwa kazini kutekeleza wajibu wa kuwalinda Watanzania wenzao. Damu yao haitamwagika bure. Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema peponi marehemu na awape nafuu askari na vijana wetu waliojeruhiwa.”
Alitumia nafasi hiyo kwa niaba ya Taifa kuwapongeza na kuwashukuru askari wa Jeshi la Polisi ambao alisema pamoja na uchache wao, juzi walifanya kazi kubwa katika mazingira magumu ya kurejesha amani bila kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu.
Aliwapongeza pia viongozi wa Mkoa na Wilaya ya Mtwara Mjini kwa uongozi mzuri. Sakata la bomba la gesi Kuhusu ujenzi huo wa bomba la gesi, Waziri Nchimbi alisema suala hilo limezungumzwa sana. Alisema Waziri Mkuu na baadhi ya mawaziri walikwenda Mtwara na Rais Jakaya Kikwete pia alilizungumzia suala hilo kwa kina.
“Mheshimiwa Spika, manufaa makubwa ambayo Mtwara itayapata yamezungumzwa sana, utaratibu wa kusafirisha kiasi kikubwa cha gesi kwa bomba ndio unaotumika duniani kote kwa sababu za unafuu wa gharama na kuhakiki ubora wake.
“Faida zake kitaifa pia zimeelezwa sana ikiwamo Taifa kuondokana kabisa na upungufu wa nishati ya umeme na umeme kupatikana kwa bei nafuu na hivyo kuharakisha mapinduzi ya viwanda na maendeleo.
“Mheshimiwa Spika, wasaliti wa Taifa letu wanajua maendeleo makubwa yatakayopatikana Mtwara na nchi yetu kutokana na gesi, hivyo wanatumia vibaya ufahamu wetu mdogo kuhusu gesi na kuchochea upinzani dhidi ya mradi huu unaotarajiwa kuwakomboa wana Mtwara na Watanzania. Watanzania na wana Mtwara lazima kwa kauli isiyoyumba tuzikatae njama hizi.
“Tunalo Taifa moja la Tanzania ambalo maliasili zake ni za Watanzania wote. Tabia iliyoanza kujengeka ya kila eneo kutaka inufaike peke yake na mali za eneo hilo italigawa taifa letu vipande vipande.
“Baadhi ya taasisi za kiraia na vyama vya siasa kwa maslahi binafsi yasiyo na upeo mpana vinaweza kudhani kuunga mkono madai ya namna hii ni kuimarisha kukubalika kwao miongoni mwa jamii, tunatimiza wajibu wetu wa kuwakumbusha msemo wa wahenga usemao “ Tamaa mbele, mauti nyuma.” Wataipasua nchi yetu, watasababisha vifo vya maelfu ya watu, watalijaza taifa vilema na majeruhi na hawatanufaika na matokeo haya mabaya.”
Aidha Waziri Nchimbi alisema vita inayofahamika kama Vita Kuu ya Afrika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyopiganwa kati ya mwaka 1998- 2003 msingi wake mkubwa ulikuwa ni kupigania rasilimali Mashariki ya nchi hiyo na ilisababisha vifo, magonjwa na njaa na Waziri Nchimbi alihoji ;
“Je, huko ndiko tunakotaka kulipeleka taifa letu?” Spika aahirisha Bunge Kutokana na tukio hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda jana alilazimika kukiahirisha kikao cha Bunge kwa siku nzima ili kupisha Kamati ya Uongozi ya Bunge kukutana ili kutathmini kwa kina kuhusu tukio hilo kabla ya kujua nini nafasi ya Bunge katika kulishughulikia.
Alisema asingeweza kuruhusu mjadala juu ya tukio hilo pamoja na kwamba lilikuwa mezani kwake kwa vile kauli za wabunge zingeweza kuchochea zaidi hali hiyo na kusababisha kutokea kwa madhara makubwa zaidi.
Alisema wakati Bunge litakapoendelea na kikao chake leo, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ndiyo itakayowasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha na kwamba majadala kuhusu hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini itapangiwa siku nyingine.
By Oscar Mbuza, Dodoma
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !