JESHI la Polisi limeanza kuwashughulikia waliotuma ujumbe wa
matusi kwa simu ya mkononi kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na
Naibu wake, Job Ndugai.
Hali hiyo imedhihirika baada ya mkazi wa Ihumwa mjini hapa,
Noel Mulingwa (26) jana kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya
Dodoma Mjini kujibu mashitaka ya kutumia lugha ya matusi kupitia
ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.
Akimsomea mashitaka, Wakili wa Serikali Farhat Seif, alidai
mbele ya Hakimu Rebeca Mbilu kuwa Februari 16 Ihumwa, mshitakiwa
alituma ujumbe wa matusi kupitia namba 0754 46..26 iliyosajiliwa kwa
jina la Anne Makinda kwa kutumia simu namba 0763 44..56 huku akijua kufanya hivyo ni makosa.
Katika mashitaka ya pili, ilidaiwa kuwa Februari 10 Ihumwa,
mshitakiwa pia alituma ujumbe wa matusi kwenye namba 076260..61 iliyosajiliwa kwa jina la Job Ndugai kwa simu namba
0763 44..56.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande hadi
Machi 21, kesi yake itakapotajwa ambapo pia Mahakama itafikiria dhamana yake.
Kiini Februari 10 viongozi wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), walitoa namba za simu za
Makinda na Ndugai ili wananchi wawashinikize viongozi hao
kujiuzulu kwa madai kuwa walikuwa wakikandamiza upinzani bungeni.
Ofisi ya Bunge kupitia kwa Katibu wake, Thomas Kashilillah
ikalitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua kali dhidi ya waliotumia lugha ya matusi kwa njia ya ujumbe mfupi au kwa kupiga simu kwa
Spika na Naibu wake.
Hata hivyo, Spika Makinda alipata kukaririwa akisema
alitumiwa ujumbe mfupi zaidi ya 400 na kupigiwa simu zisizopungua 200,zilizokuwa zikimkashifu na nyingine zikimtisha, huku Naibu
Spika akipokea ujumbe na simu kadhaa zenye matusi.
Awali Jeshi la Polisi lilidai kuwa, Mlingwa alikamatwa
Februari 12 katika eneo la sekondari ya City mjini hapa kwa tuhuma za kutuma ujumbe wa maandishi wenye vitisho na matusi kwa Spika
wa Bunge la Tanzania na Naibu wake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alitoa
mwito kwa wananchi wote wa mkoa wa Dodoma kuacha kutumia simu zao za mkononi kwa kutuma ujumbe wa matusi na vitisho
kwa watu wengine; yeyote atakayefanya hivyo atakamatwa na atafikishwa katika vyombo vya sheria.
BY SIFA LUBASI, DODOMA
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !