Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Chadema,Wilfred Lwakatare
|
Dar es Salaam. Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa
Chadema,Wilfred Lwakatare jana alikamatwa, akahojiwa na kupekuliwa na polisi
kwa tuhuma za uchochezi wa uvunjifu wa amani.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso aliliambia
Mwananchi jana kuwa Lwakatare alikamatwa kutokana na taarifa zilizopatikana
kutoka katika video kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha akiwahamasisha
watu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani au uhalifu. Alipoulizwa mahali na
lini alikamatwa Lwakatare, Senso alisema hilo halijalishi, lakini jambo la
msingi ni kwamba wako naye kwa ajili ya uchunguzi na hakutaka kuweka bayana ni
lini wangemwachia.
Siku nzima ya jana mitandao ilikuwa imetawaliwa na habari ya
picha ya video ikimwonyesha Lwakatare akidaiwa kupanga mikakati ya kumteka
Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Dennis Msacky. Lwakatare alionekana akitoa
maelekezo kwa watu, ambao sura zao hazikuonekana, akiwataka kufuatilia nyendo
za Msacky.
Alionyeshwa akiwataka watu hao kumkamata bila ya kumdhuru
Msacky, lakini wamtupe mbali kama njia ya kumnyamazisha. Alikuwa anamtuhumu
Msacky kama alikuwa anashirikiana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe
ili kukihujumu chama chao.
“Inabidi mfahamu nyendo za mtu huyu, kama anapenda vitu kama
kutembea usiku au kinywaji anachokunywa,” alinukuliwa kwenye mtandao huo.
Pia anaonekana kwenye video hiyo akitoa mbinu mbalimbali za
namna ya kufanya utekaji nyara.
Wakili wa Lwakatare alonga
Wakati akihojiwa na kupekuliwa, Lwakatare aliongozana na
wakili wa kujitegemea, Nyaronyo Kicheere, ambaye alilieleza Mwananchi kuwa
mteja wake alichukuliwa kutoka ofisini kwake kwenye Makao Makuu ya Chadema
yaliyoko Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kicheere alidai kuwa hakuwa na uhakika kuwa Lwakatare
alikamatwa muda gani ofisini kwake kwani yeye aliitwa Makao Makuu ya Jeshi la
Polisi saa 9.00 alasiri.Mwananchi, hata hivyo, lina taarifa kuwa Lwakatare
alikamatwa na askari wanne saa 7.00 mchana na kupelekwa Makao Makuu ya Polisi.
Lwakatare, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba
Mjini kupitia CUF na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alipokamatwa
alifuatana na maofisa kadhaa wa Chadema akiwamo Ofisa wa Ulinzi wa chama hicho,
Hemed Sabula na Ofisa wa Mawasiliano aliyejulikana kwa jina moja tu la
Karungebe.
Alichukuliwa ndani ya gari aina ya Land Cruiser na kupelekwa
moja kwa moja Makao Makuu ya Jeshi la Polisi katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Mahojiano
Kicheere alisema Lwakatare alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi
ingawa alidai polisi hawakubainisha ni uchochezi upi.
Mahojiano hayo kwa Lwakatare yaliongozwa na Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP) Obadia Jonas.
“Lwakatare alihojiwa kuanzia saa 9.00 alasiri hadi 9.55
jioni na tuhuma zilizomkabili ni uchochezi. Ila askari hawakuniambia ni
uchochezi upi,” alieleza Kicheere. Alisema kuwa baada ya mahojiano yale
waliamriwa kwenda nyumbani kwa Lwakatare kwa ajili ya upekuzi.
Upekuzi
Lwakatare, ambaye anaishi eneo la Kimara King’ong’o jijini
Dar es Salaam, alisindikizwa na askari saba walioongozwa na ACP Jonas. Katika
msafara huo wa kwenda kupekua nyumbani kwake, maofisa wa Chadema walizuiwa
kuongozana naye, isipokuwa mwanasheria wake, Kicheere, ndiye aliruhusiwa
kuongozana naye.
“Tunavyoongea na wewe hivi sasa ni kwamba upekuzi unaendelea
katika vyumba vya nyumba . Kwa sasa tuko ndani ya chumba chake cha kulala,”
alieleza Kicheere.
Kicheere alisema upekuzi huo ulianza saa 10.30 jioni na
ulilenga katika kutafuta nyaraka ambazo zingeweza kutumika kama ushahidi wa
tuhuma hizo. Alisema kuwa baada ya kumalizika kwa upekuzi kilichokuwa
kinatakiwa kufuata ni kuandikisha maelezo katika Kituo cha Kikuu cha Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
“Hawa jamaa wanaendelea na upekuzi na hawajapata kitu
chochote muda huu tunavyoongea na wewe. Ila tukimaliza tutarudi Kituo Kikuu cha
Polisi kwa ajili ya kuandikisha maelezo,” aliongeza Kicheere.
Dk Slaa anena
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema polisi
walifika katika ofisi za chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam na kuomba
kuzungumza na Lwakatare.
“Ni kweli polisi wamefika hapa na kuomba kuzungumza na
Lwakatare, ila walichokizungumza mimi sikijui kwa kweli,” alisema Dk Slaa.
Alipoulizwa kama polisi hao waliondoka na Lwakatare na wapi
walikompeleka alisema, “Nadhani ofisi yangu unaijua jinsi ilivyo, mimi nikiwa
ndani ya ofisi yangu ni vigumu kugundua kinachoendelea katika ofisi nyingine,
kwa hiyo sijui hilo.”
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !