‘Mwanajeshi’ wa Chadema aishi na ‘sangoma’ - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » ‘Mwanajeshi’ wa Chadema aishi na ‘sangoma’

‘Mwanajeshi’ wa Chadema aishi na ‘sangoma’

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Monday, January 7, 2013 | 2:22 PM

Abubakari Kikuru
Pichani kushoto ni Mbunge Lema (shati jeupe) na kulia kabisa mwenye shati jeupe ni Mbunge Nasari

SHABIKI wa Chadema aliyepiga picha na baadhi ya wabunge wa chama hicho akiwa amevalia kijeshi amekuwa akiishi na mganga wa kienyeji, imebainika.

Abubakari Kikuru, 29, ambaye amekamatwa na kufunguliwa jalada namba MOS/ IR/94/2013 katika kituo kikuu cha Polisi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ni mzaliwa wa Lushoto, Tanga na si askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kama ilivyokuwa ikidhaniwa awali.

Taarifa iliyotolewa jana na JWTZ ilisema Kikuru alikamatwa Januari 3 saa 5.30 asubuhi eneo la Bomang’ombe, Kilimanjaro na alipopekuliwa nyumbani alikokuwa anaishi na mganga huyo Matoroka Rashid, alikutwa na sare za Jeshi ambazo ni kofia mbili, suruali moja na majampa mawili.

Bomang’ombe iko Wilayani Hai ambako ndiko anakotoka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

“Uchunguzi zaidi pamoja na taratibu za kufikishwa mahakamani zinashughulikiwa na Jeshi la Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro,” ilisema taarifa na kuvionya vyama vya siasa kutoiga mfano wa Chadema wa kukubaliana na watu wanaojitambulisha kuwa ni askari, “mtazamo huu si sahihi kwani ni uvunjifu wa Katiba na sheria.”

Pia iliviasa vyombo vya habari kuwa vinafanya uchunguzi kabla ya kuchapisha habari za mtazamo huo, bila kusahau kuwa vyenyewe ni sehemu ya Taifa na vinastahili kudumisha amani.

“JWTZ inachukua fursa hii kuwakumbusha wananchi, kutoshabikia jambo kama hili lililojitokeza kwani kufanya hivyo ni kuvunja Katiba ya nchi yetu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Desemba 24, 2012 gazeti la Mwananchi katika ukurasa wake wa kwanza liliandika habari ikiwa na picha ya mtu aliyetambulishwa kuwa askari wa JWTZ, kambi ya Monduli, Arusha akiwa na wabunge, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Joshua Nasari (Arumeru Mashariki) baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Wabunge hao katika mji mdogo wa Mererani, Simanjiro mkoani Manyara.

Baada ya kuonekana taarifa hiyo katika gazeti hilo, JWTZ ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kutokana na kushitushwa na taarifa hizo, ikieleza bayana kwamba uchunguzi wa kina unafanyika, ili kutambua kama mtu huyo ni askari wa kweli au la.

JWTZ ilitoa taarifa ya kufanya uchunguzi kwa sababu, kwanza jina la mtu huyo halikuandikwa, pili kikosi halisi cha mtu huyo hakikuandikwa, lakini pia ilitia shaka kuwa sare alizovaa ikionesha kuwa ni vazi la JWTZ hazikuwa sahihi.

Kimsingi ilitia shaka kutokana na mavazi hayo kutofautiana na mavazi halisi ya JWTZ kwa sasa, kama ilivyoonesha katika picha hiyo. Pia haikuwa rahisi kumtambua mtu huyo kutokana na kuficha sehemu ya uso wake kwa kofia.

JWTZ ilitoa taarifa kuwa itakapobaini ukweli huo, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kutokana na Kanuni za Majeshi ya Ulinzi, kwani kwa mujibu wa sheria namba nne (4) ya mabadiliko ya nane (8) katika Katiba ya nchi ya mwaka 1992 ibara ya 147(3), mwanajeshi yeyote hatakiwi kujihusisha na masuala ya siasa.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger