Zitto aingia matatani - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » Zitto aingia matatani

Zitto aingia matatani

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Saturday, January 12, 2013 | 10:59 PM

Kwa ufupi
RAIA WA KIGENI ATAKA KUMSHTAKI KWA TUHUMA ALIZOZITOA BUNGENI, YEYE AKIMBILIA KWA KATIBU WA BUNGE


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ameingia matatani, baada ya kutakiwa kukanusha tuhuma alizozitoa bungeni katika Mkutano wa Tisa wa Bunge, kwamba mfanyabiashara wa kigeni, Moto Mabanga, alipewa vitalu vya mafuta kinyume na taratibu.

Mfanyabiashara huyo amesema kuwa iwapo Zitto atashindwa kukanusha tuhuma hizo, atafikishwa mahakamani.

Barua iliyoandikwa kwenda kwa mbunge huyo iliyosainiwa na Mwanasheria wa Mabanga, Lawley Shein wa Kampuni ya Uwakili ya Lawley Shein Attorneys, ambayo Mwananchi Jumapili limeiona, inaeleza kuwa hoja binafsi aliyoitoa Zitto, haikuwa na ukweli wowote.

Barua hiyo ya tarehe 28 Novemba, 2012 ilisema kuwa hoja hiyo ya Zitto ni ya uongo, imemkashifu mteja wao na kumshushia hadhi yake binafsi na biashara zake.

“Katika kuthibitisha kuwa tuhuma zako siyo za kweli katika hoja uliyotoa, umemtaja mteja wetu kama raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mteja wetu ni raia wa Afrika Kusini, lakini, umeamua kumtaja kama raia wa Kongo bila kuangalia ukweli,” alisema Shein.

Katika barua hiyo, Shein pia amesema kuwa Zitto amemtuhumu mteja wake Mabanga kuwa aliwahonga baadhi ya vigogo serikalini na kuwapa rushwa wanasiasa katika mchakato wa kufanikisha upatikanaji wa vitalu hivyo.

“Tuhuma hizo siyo za kweli, mteja wetu alifuata taratibu zote kwa uwazi na mamlaka husika nchini na hakuwahi kutoa rushwa kwa mtu yeyote,” alisema mwanasheria huyo.

“Tuhuma hizi ni za uongo, zimemharibia jina mteja wetu na kumsababishia madhara. Kama hutazifuta kauli hizo, uongo huo utamsababishia mteja wetu madhara makubwa zaidi na tutalazimika kudai fidia,” Shein alionya kupitia barua hiyo.

Shein aliongeza kuwa pamoja na Zitto kuongea hoja hiyo akiwa bungeni hivyo kuwa na kinga ya kibunge, lakini kwa mazingira aliyotolea hoja hiyo alitumia vibaya kinga ya kibunge, anayopata mbunge yeyote anapotoa hoja akiwa bungeni.

Kupitia barua hiyo, Shein alimtaka Zitto kufuta kauli yake dhidi ya mteja wao na kwamba mteja wao ana haki zote za kushtaki dhidi ya hoja hiyo.

Zitto azungumza
Alipotakiwa kuzungumzia hoja hiyo na hatua atakazochukua, Zitto alisema kuwa amemwandikia barua Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, kumjulisha hatua hiyo ya kutaka kushtakiwa.
“Nimemwandikia Katibu wa Bunge kumjulisha kwamba nimeletewa kusudio la kushtakiwa, maana hili ni suala la Kinga ya Bunge,” alisema Zitto na kuongeza:

“Mbunge ana kinga kwa masuala aliyozungumza ndani ya Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 100 ya Katiba. Kwa hiyo Katibu (Dk Kashililah), atawajibu hao wanasheria.”

Ibara hiyo ya 100 (2) inaeleza kuwa; Bila ya kuathiri Katiba au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo alilosema au kulifanya ndani ya Bunge, au alilolileta bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo.

Naibu Spika
Kwa upande wake Naibu Spika, Job Ndugai alisema kuwa hana taarifa za kusudio hilo la kutaka kushtakiwa kwa Zi tto, lakini akasema kwamba mbunge ana kinga ya Bunge pindi akitoa hoja au wazo lolote, akiwa ndani ya Bunge.

Ndugai alisema kuwa kutokana na mabadiliko madogo ya sheria yaliyofanyika, mwananchi anaweza kuandika barua kwa Spika wa Bunge kutokana na tuhuma alizotoa mbunge dhidi yake bungeni.
“Mtu anaweza kuandika barua kwa Spika na Spika ataona hatua zaidi za kuchukua za kibunge,” alisema Ndugai.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger