WIZARA ya Ujenzi imetakiwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa barabara za lami - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » WIZARA ya Ujenzi imetakiwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa barabara za lami

WIZARA ya Ujenzi imetakiwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa barabara za lami

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Saturday, January 12, 2013 | 8:07 AM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete    
Kwa ufupi

‘‘Naomba sana barabara hizi zinazojengwa hapa Tabora na kwingineko zisimamiwe vizuri kuanzia hatua ya mwanzo ili zidumu kwa muda wa miaka 15 kabla ya kufanyiwa ukarabati,

WIZARA ya Ujenzi imetakiwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa barabara za lami hapa nchini ili zijengwe kwa kiwango bora, badala ya kuwaachia makandarasi wajenge na kisha kukabidhi bila ya kujiridhisha kiwango cha barabara husika.

Rai hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya lami kutoka Tabora-Urambo kupitia Ndono baada ya jana yake kuweka jiwe la msingi katika Barabara ya Nzega-Tabora kupitia Puge na Tabora-Itigi kupitia Nyahua.

Akizungumza na wananchi, Rais Kikwete alisema kuwa barabara nyingi zinazojengwa hapa nchini zinaharibika mapema kwa sababu ya kutokuwa na usimamizi mzuri kuanzia hatua za mwanzo za ujenzi mpaka mwisho wake.

‘‘Naomba sana barabara hizi zinazojengwa hapa Tabora na kwingineko zisimamiwe vizuri kuanzia hatua ya mwanzo ili zidumu kwa muda wa miaka 15 kabla ya kufanyiwa ukarabati, baada ya hapo ndiyo tufikirie kuzifanyia ukarabati, na siyo barabara itengenezwe na kuharibika kabla ya mwaka kwisha,’’ alisema Rais.

Alisema kitendo cha barabara ya lami kujengwa leo na kuharibika ndani ya kipindi kifupi ni hasara kwa uchumi wa taifa, haifai na mkandarasi wa namna hiyo hafai kupewa tenda tena na kumtaka waziri Magufuli aendelee kuwashughulikia wazembe.

Rais Kikwete aliongeza kuwa, Serikali inatumia fedha nyingi kujenga barabara kwa kiwango cha lami, lengo likiwa ni kuharakisha shughuli za kimaendeleo, kwani barabara nzuri ni kigezo kikubwa cha kuinua uchumi kwa sababu usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka sehemu moja kwenda nyingine unakuwa mwepesi.

“Tafadhali sana, Wizara ya Ujenzi simamieni vizuri hizi barabara ili zidumu, hawa makandarai wasifanye wanavyotaka wao bali wafanye kile tunachotaka sisi. Naagiza walipwe hela zao na zile zitakazobakia watalipwa mwezi wa sita mwaka huu ili kazi hii iende haraka iwezekanavyo,” alisema Rais Kikwete.

Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli, alisema kuwa ujenzi wa barabara za Mkoa wa Tabora kwa kiwango cha lami unatakiwa kukamilika ndani ya miezi 16 kuanzia sasa, hivyo akaagiza kila mkandarasi anayetengeneza barabara hizo kukamilisha kazi yake kwa wakati vinginevyo atafukuzwa kama walivyofukuzwa makandarasi wengine.

“Tanzania siyo mahali pa kujifunzia ukandarasi wa barabara, Serikali ya Rais Jakaya Kikwete iko makini, inahangaika kutafuta fedha usiku na mchana, halafu mtu mmoja atafune hela yetu bure kwa kutufanyia kazi za ovyoovyo ….hili halikubaliki, tutawashughulikia”, alisema Dk Magufuli.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger