Kinana akumbana na hujuma ya kukaa gizani - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » Kinana akumbana na hujuma ya kukaa gizani

Kinana akumbana na hujuma ya kukaa gizani

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Sunday, February 3, 2013 | 8:35 PM



Kwa ufupi

Huku kukiwa giza nene, mafundi wa Tanesco wa Wilaya ya Kibondo wakiongozwa na meneja wao, Dawson Lupenza walifanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya mji huo na kugundua kuwa kulikuwa na hujuma.

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana aliyekuwa katika Wilaya ya Kibondo juzi na jana alipata wakati mgumu baada ya watu wasiojulikana kudaiwa kufanya hujuma kwa kuzima umeme mji mzima.

Umeme ulizimwa na watu wasiojulikana juzi  kuanzia saa 5.00 usiku hadi jana saa 4.00 asubuhi baada ya mafundi wa Tanesco kugundua hujuma hiyo.
Umeme huo ulizimwa mara baada ya Kinana kuzungumza na viongozi wa CCM katika kikao cha ndani.

Huku kukiwa giza nene, mafundi wa Tanesco wa Wilaya ya Kibondo wakiongozwa na meneja wao, Dawson Lupenza walifanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya mji huo na kugundua kuwa kulikuwa na hujuma.

Mafundi hao katika eneo la hujuma walibaini waya wa copper ulifungwa na mawe mawili yaliyosaidia kuurusha katika nyaya za Tanesco na kusababisha umeme kuzimika.

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Venance Mwamoto ambaye alikuwa bega kwa bega na mafundi Tanesco, alisema anahisi hiyo ni hujuma iliyofanywa na mtu au kikundi cha watu ili kukwamisha ziara ya Kinana.

Mwamoto alisema vyombo vya dola vitafanya kazi usiku na mchana ili kuwabaini waliofanya hujuma hiyo.

“Hawa ni maadui zetu wakubwa, wamezima umeme mji mzima huku kikiwa na ugeni wa katibu mkuu, tutawasaka popote hadi tuwapate,” alisema Mwamoto.

Alisema wamechukua nyaya na mawe zilizotumika kuzima umeme huo kwa ajili kupima alama za vidole ili kufanya uchunguzi zaidi.

Aidha, Mwamoto alisema kwa mazingira yaliyopo huenda hujama hiyo imefanywa na wafuasi wa vyama vya upinzani.

“Nadhani umeona mikutano ya jana ilivyofana, Kinana ameiteka Kibondo nzima sasa wenzetu wa upinzani huenda wamekasirishwa na hilo sasa wanaamua kuhujumu,”alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa Tanesco Wilaya ya Kibondo, Lupenza alisema hii ni mara ya pili kufanywa hujuma kama hiyo.

Alisema mara ya kwanza hujuma hiyo ilifanywa Desemba 26,mwaka jana wakati wananchi walikuwa katika sherehe za Krismasi.

“Hujuma hii imefanywa na mtaalamu wa masuala ya umeme anayeelewa nini anachokifanya. Tunahitaji ushirikiano kudhibiti hali hii,” alisema Lupenza.

Alisema mbali na ugeni wa katibu mkuu, wananchi wa mji huo wamepata usumbufu kutokana na kukatika umeme katika eneo hilo ambalo halijawahi kuwa na umeme wa mgao.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger