KINARA wa vurugu za kidini zinazoibuka kila siku ya Ijumaa jijini Dar es Salaam, amejulikana. - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » KINARA wa vurugu za kidini zinazoibuka kila siku ya Ijumaa jijini Dar es Salaam, amejulikana.

KINARA wa vurugu za kidini zinazoibuka kila siku ya Ijumaa jijini Dar es Salaam, amejulikana.

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Thursday, February 21, 2013 | 7:40 PM

•  Polisi watangaza bingo atakayesaidia kumpata
na Farida Ramadhani   

KINARA wa vurugu za kidini zinazoibuka kila siku ya Ijumaa jijini Dar es Salaam, amejulikana.

Kinara huyo ametajwa kuwa ni Sheikh Issa Kondo Bungo ambaye amekuwa akitafutwa na polisi kwa muda mrefu bila mafanikio.

Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, zilisema kuwa Sheikh Bungo anadaiwa kuhusika na matukio kadhaa makubwa ya vurugu za kidini, zilizotokea kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam.

Duru za kipolisi zilitaja baadhi ya matukio ambayo Sheikh Bungo anadaiwa kuhusika nayo kuwa ni pamoja na tukio la kuchoma moto kanisa la TAG la Mbagala, baada ya mtoto (jina limehifadhiwa), kukojolea Qur’an.

Tukio la kukojolea kitabu hicho lilitokea Oktoba 10 katika eneo la Chamazi saa 10 jioni wakati watoto hao wakiwa katika ‘kijiwe’ chao cha kuchezea mpira.

Vurugu hizo zilisababisha kuvunjwa kwa vioo vya magari, madirisha ya makanisa pamoja na kuibwa kwa vifaa vya kwaya katika makanisa hayo ambayo ni ya Anglikana, Wasabato na Pentekoste.

Kutokana na tukio hilo ambalo liliibua vurugu kubwa kutoka kwa baadhi ya waumini wa Kiislamu wanaojiita wenye msimamo mkali, Sheikh Bungo anatajwa kuhusika kushawishi wenzake kuchoma kanisa hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Jeshi la Polisi limekuwa likimsaka kwa muda mrefu, lakini halijafanikiwa kumtia mbaroni kutokana na staili yake ya kuishi kwani hana makazi maalumu.

“Shekh huyo pia anahusika kushawishi wafuasi wa Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Ponda Issa Ponda kuandamana kila siku ya Ijumaa ili kushinikiza mahakama itoe dhamana kwa Ponda ambaye kwa sasa yuko rumande akikabiliwa na kesi ya uchochezi,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Kwa mujibu wa habari hizo, tangu tukio la vurugu za Mbagala lilipotokea, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata wafuasi wa sheikh huyo na wengine wako mahakamani, lakini yeye hajapatikana.

Tayari Sheikh Bungo pamoja na wenzake wamefunguliwa kesi namba THA/ IR/ 7794/ 2012 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

“Mwaka huu tumeshamfungulia jalada lingine namba CHA/ RB/ 10652013 katika kituo cha polisi cha Chang’ombe, hivyo tunawaomba wananachi wanaopenda amani watoe taarifa katika kituo chochote cha polisi endapo ataonekana,” alisema mtoa habari wetu.

Hadi sasa polisi imemfikisha mahakamani Shekh Ponda pamoja na wenzake 49 ambao kesi zao zinaendelea kusikilizwa huku wakiendelea kukamata wengine kila vurugu hizo zinapotokea.

Vurugu hizo ambazo zimekuwa zikiwatia hofu wakazi wengi jijini Dar es Salaam na nchi nzima kwa ujumla, zimekuwa na tabia ya kuibuka kila siku ya Ijumaa na siku ambazo kesi ya Sheikh Ponda inapotajwa.

Hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya shughuli za kimaendeleo katika jiji hilo kusimama kwa muda, huku polisi wakilazimika kutumia nguvu kubwa kuweka ulinzi.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger