SERIKALI MBIONI KUMILIKI HISA ASILIMIA 100 ZA TTCL - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » SERIKALI MBIONI KUMILIKI HISA ASILIMIA 100 ZA TTCL

SERIKALI MBIONI KUMILIKI HISA ASILIMIA 100 ZA TTCL

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Tuesday, February 12, 2013 | 1:08 PM

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Mhe. Januari Makamba
 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Serikali imeanza mchakato wa kumiliki Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa asilimia 100  ikiwa ni njia mojawapo ya kufanya mageuzi ya kibiashara na kuliendesha shirika hilo kisayansi zaidi ya ilivyo sasa.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Mh. Januari Makamba aliyasema hayo mkoani Dodoma mwanzoni mwa wiki hii wakati akielezea mikakati mbalimbali inayotaka kuchukuliwa na serikali ili kuweza kulimiliki shirika hilo kwa asilimia 100 badala ya 65 za sasa.

Kwa sasa TTCL inamilikiwa kwa ubia, serikali ikiwa na asilimia 65 wakati 35 zinamilikiwa na kampuni ya simu za mikononi ya Airtel.

“Mazungumzo tayari yameshaanza na dhamira yetu ni kununua aslimia 35 ya hisa zinazomilikiwa na wenzetu ili serikali iweze kumiliki asilimia 100,” alisema Mh. Makamba.

Alisema katika kufanya mipango ya kwenda mbele kimaendeleo kupitia shirika hili ni lazima kufanya mchakato wa kulimiliki kwa asilimia 100 ili serikali iweze kufanya mageuzi kwa utashi wake kadiri inavyofaa.

Alifafanua kwamba hatua hii ni Kutokana na changamoto zilizopo za kimuundo, kiungozi na ndio maana serikali imechukua hatua za kinidhamu miongoni mwa baadhi ya watendaji waliobainika kutumia madaraka yao vibaya ikiwa ni pamoja na kufanya ubadhirifu na hivyo kulisababishia shirika hasara.

“Hii ni moja ya hatua muhimu katika kuelekea kufanya mageuzi katika shirika hili kongwe hapa nchini,” alisema.

Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni matatizo ya mtaji, na kusema kuwa ni lazima yashughulikiwe ikiwa ni pamoja na kwenda na teknolojia mpya na kulifanya shirika lijiwekeze kibiashara zaidi ya ilivyo sasa.

“Naamini katika kufanya mageuzi makubwa bodi itachukua nafasi yake kwa maana ya uongozi wa shirika katika kurekebisha mambo na mapungufu yaliyopo, kwa maana ya kuweka uongozi mpya utakaoleta mabadiliko ili kulibadilisha liwe shirika kubwa la kisasa linalotengeneza faida,” alisisitiza.

Alisema kutokana na historia yake huko nyuma kampuni hii ilipaswa kuwa ndio kampuni inayoongoza kimapato na pia kwa kutoa huduma nchi nzima kutokana na kuwa ipo kila wilaya katika nchi, lakini kutokana na changamoto mbalimbali imekuwa ni tofauti na matarajio yaliyowekwa wakati huo.

Alisisitiza kuwa wakati sasa umefika kwa shirika kuwa katika mtazamo wa kuwekeza kibiashara zaidi na ushindani.

“Shirika hili kongwe limeendelea kubaki kama lilivyo na serikali imeliona hilo, kinachohitajika ni kuwekeza katika rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na ushindani wa kibiashara uliopo sasa,” aliongeza.

Alisema mbali na changamoto zote hizo lakini TTCL imefanikiwa kuunganisha Ofisi za Serikali, mashirika mbalimbali, Taasisi za kifedha, utangazaji na Taasisi za elimu na hivyo kuboresha matumizi ya huduma za mtandao wa mawasiliano kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.

“Kwa mfano huduma za video conferencing zinawezesha kuendesha mafunzo au mikutano kwa wahusika na hivyo kuongeza ushiriki, na kupunguza gharama,” alisema.

Akisikiliza kero za wafanyakazi wa kampuni hiyo hivi karibuni, waziri Makamba aliiagiza bodi ya Wakurugenzi ya TTCL kumtumia Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa mahesabu ili kuthibitisha tuhuma za ubadhirifu wa fedha za kampuni hiyo ili hatua za kisheria wakibainika.

Baadhi ya malalamiko yaliyotolewa na wafanyakazi hao ni pamoja na uongozi na bodi dhaifu katika ufuatiliaji mambo, ubadhirifu wa fedha za kampuni pamoja na uhamisho wa wafanyakazi usofuata taratibu.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger