Treni ikiwasili Jijini Mwanza leo |
MWANZA, TANZANIA
MAMIA ya wakazi wa jiji la Mwanza, walilipuka kwa shangwe na
vigelegele wakati wakiilaki Treni ya Abiria iliyowasili hapa kwa mara ya
kwanza baada ya kusitishwa kwa safari zake toka Disemba 2009.
Treni hiyo iliwasili katika Stesheni ya mjini Mwanza saa 5:55 mchana,
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba akiwa ni mmoja wa abiria
waliopokewa na wananchi hao walioongozwa na Mkuu wa wilaya ya Nyamagana,
Baraka Konisaga.
Huku baadhi wakiwa na mabango yaliyobeba ujumbe mbalimbali wa kuipongeza
Serikali na Waziri wa Uchukuzi Dk Halson Mwakyembe, wananchi hao
walianza kushangilia mara tu Treni hiyo ilipotokeza kwenye yadi ya
stesheni.
Shangwe hizo zilipokewa na abiria waliokuwemo ambao walionyesha nyuso za
furaha na kuwapungia mikono wananchi na viongozi hao wakiwemo ndugu na
jamaa waliokuwa wamefika kuwapokea.
“Hayawi hayawi leo yamekuwa, wao wao Treni ya abiria kuja Mwanza” ndivyo
baadhi ya wananchi walivyosikika wakiimba wakati Dkt Tizeba akishuka
pamoja na abiria wenzake na kupokewa na viongozi wa Chama na Serikali.
Pamoja na Konisaga aliyekuwa akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
Mhandisi Evarist Ndikilo, wengine waliipokea Treni hiyo ni pamoja na
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amina Masenza, Meya wa Jiji la Mwanza
Stanslaus Mabula na Katibu wa CCM Wilayani Nyamagana, Deogratias Rutta.
Baadhi ya abiria wakiwemo Mwaka Hussin mkazi wa Tabora na Moshi Mfalila
mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es salaam , wakizungumza na Uhuru
walisema kuwa wanaishukuru serikali kurejesha usafirii huo wa wanyonge.
“Tunaishukuru serikali usafiri huu mzuri, japo viti vya mabehewa naona
vimechoka, waviboreshe na kudhibiti vibaka wasiingie ovyo.” Alisema
Hussein huku Mfalila akidai kuwa waboreshe Injini za usafiri huo ili
abiria wasikwame tena kama walivyokwama juzi kwa saa nne, Ubungo.
Wakazi wa jiji la Mwanza waliofika kuilaki Treni hiyo, wakiwemo Sikitu
Chibulule, Nelson Wilson na Mwanaidi Rajabu, walimshukuru Rais Jakaya
Kikwete kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa ya kufufu usafiri wa Reli na
kusema kuwa serikali ya CCM sasa inafurahisha kwa uchapa kazi.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL nchini,
Kipallo Kisamfu alisema kuwa, shirika lake lina furaha isiyo kifani
kuwasili kwa Treni hiyo Mwanza, siku ambayo ina historia ya miaka 51
Uhuru wa Tanzania Bara.
“Disemba 2009 niyo ilikuwa mara ya mwisho Treni hii kuja Mwanza safari
zake zikasitishwa, lengo letu ni kurudisha ufanisi wa Treni uliokuwepo
awali, lengo hilo si jepesi ni zito lakini kwa hali tuliyofikia tutafika
huu ni mwanzo tu wa jitihada za serikali yetu.” Alisema Kisamfu.
Alieleza kuwa mpango wa serikali ni kuhakikisha Treni inafufuka na kutoa
mchango wake mkubwa katika huduma za jamii na kukuza pato la taifa,
hivyo pamoja na kuanza na mabehewa machache, huduma hiyo itaboreka siku
hadi siku kwani ukarabati wa mabehewa mengine na vichwa vya Treni,
unendelea.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !