UTAFITI: Watoto wa kike wanaelewa haraka darasani kuliko wa kiume - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » UTAFITI: Watoto wa kike wanaelewa haraka darasani kuliko wa kiume

UTAFITI: Watoto wa kike wanaelewa haraka darasani kuliko wa kiume

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Friday, January 18, 2013 | 10:08 PM

Kwa ufupi

“Wasichana ni wasikivu na waelewa na ikitokea ana tatizo ni rahisi kukufuata kutaka ushauri na wakati mwingine ni rahisi kumsaidia akihitaji msaada,
tofauti na wavulana ambao ni nadra kuuliza jambo baada ya mwalimu kutoka darasani, hata kama hajaelewa,”

Wanafunzi wa kike 

UTAFITI mpya wa masuala ya elimu umebainisha kwamba wanafunzi wa kike hufanya vizuri zaidi darasani kuliko wanafunzi wa kiume.

Matokeo ya utafiti huo, uliofanywa hivi karibuni na wataalamu wa elimu kutoka vyuo vikuu vya Georgia na Columbia vya nchini Marekani, umebaini kuwa watoto wa kike wa kati ya umri wa miaka sita hadi 12, huelewa kwa haraka darasani kuliko watoto wale wa  kiume.

Wameeleza kuwa wanafunzi hao wa kike huwa makini zaidi kumsikiliza mwalimu anapokuwa akifundisha darasani, tofauti na watoto wa kiume, ambao hutumia muda mwingi kufanya mambo mengine ikiwamo kucheza, kuchokozana na pengine kugombana wao kwa wao.

Matokeo hayo yaliyochapishwa katika Jarida la Rasilimali Watu la Marekani na kuandikwa kwenye mtandao wa Daily Mail, yanaonyesha kuwa utafiti huo uliangalia uwezo wa watoto zaidi ya 5,000 katika Kusoma, Hisabati na Sayansi.

Watafiti hao kwa kuangalia alama za majaribio mbalimbali na maoni ya walimu, waligundua kuwa hata katika hatua za awali (chekechea), alama za watoto wa kike zimekuwa juu siku zote ikilinganishwa na alama za watoto wa kiume.

Mmoja wa watafiti hao, Christopher Cornwell, anasema kuwa ujuzi wa wanafunzi hao, ndiyo njia kubwa inayotumiwa na walimu kuwapanga wanafunzi wao katika madaraja.

Aliongeza kuwa kuna vigezo sita vya kupima uwezo wa watoto, ambavyo ni: Usikivu, ufuatiliaji wa kazi anazopewa darasani, kupenda kujifunza, kusoma kwa kujitegemea, uwezo wa kubadilika kutokana na mazingira na mpangilio wa mambo yake.

“Nafikiri kwa mtu yeyote ambaye ni mzazi mwenye mtoto wa kike na kiume, atakubaliana nami kuwa watoto wa kike wako mbele katika mambo yote hayo,” anasema Cornwell.

Cornwell aliongeza kuwa matokeo ya utafiti huo yamewapa mwanga kujua kwa nini hivi sasa asilimia 60 ya wahitimu wa shahada ya kwanza nchini Marekani ni wanawake na kwamba hali hiyo itasababisha wanaume kuwa na wakati mgumu kwenye soko la ajira.

Wizara ya elimu
Mkuu wa Elimu wa Kitengo cha Uratibu ,Ushauri na Unasihi katika Shule na Vyuo vya Ualimu kutoka Wizara ya ELimu na Mafunzo ya Ufundi, Franaeli Munishi, anasema kuwa anaunga mkono utafiti huo akisema kuwa hiyo ni kulingana na matokeo ya hivi karibuni na kwamba wasichana wamekuwa wakifanya vizuri, ingawa mara nyingi elimu yao ni ya kujituma zaidi tofauti na wavulana.

Anasema kuwa hata kwenye baadhi ya tafiti za kielimu ambazo amezifanya, amebaini kuwa baadhi wa walimu hupata wakati mgumu wanapowafundisha wavulana kuliko wasichana kutokana na wavulana kuwa wasumbufu.

Anaongeza kuwa sababu kubwa inayowafanya wasichana wafanye vizuri ni kuwa wasikivu, lakini pia kuwa wazuri katika  lugha na kwamba kwa lugha ni kila kitu kwenye masomo ni lazima watafanya vizuri tofauti na wavulana, ambao ni wazuri kwenye masomo kama Hesabu na Sayansi.

“Sababu kubwa ya wasichana kuwa wasikivu darasani inatokana na malezi yao kwa kuwa muda mwingi, wapo karibu na  mama zao tofauti na wavulana, ambao muda mwingi huwa na mambo yao kitu kinachowafanya wajilee wenyewe na kujiamulia mambo yao,” anasema Munishi.

Naye Mratibu Msaidizi Kitengo Cha Ushauri na Unasihi katika Shule na Vyuo vya Ualimu wizarani hapo, Madina Kemilembe anakubaliana na utafiti huo ingawa anasema siyo kwa asilimia 100 kwa kuwa hajafanya utafiti kama huo.

Anasema kuwa katika baadhi ya mikoa yenye shughuli nyingi za kibiashara, wavulana hupotea kabisa kutokana na kutokuwa wasikivu darasani jambo linalowafanya walimu wachoke kuwafuatilia, hivyo kutumia muda wao mwingi kuwafuatilia wasichana wanaoonyesha kujali na umakini kwenye masomo.

“Katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa au yenye migodi, wavulana ndiyo hupotea kabisa kutokana na tabia yao ya kutokuwa wasikivu darasani kwani walimu wanawaona mizigo kwa sababu ni watukutu na wenyewe huamua kwenda kujihusisha na shughuli za kutafuta fedha,” anasema  Kemilembe na kuongeza:
“Matokeo yake, sehemu kama hizo wanaobaki shuleni ni wasichana pekee na hii ndiyo huwafanya wasichana wafanye vizuri.”

Anasema kuwa hata katika mazingira ya kawaida tangu  zamani wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja; kumsikiliza mtu na kumwelewa kuliko mvulana na linapokuja suala la elimu hali inakuwa hivyo hivyo.

Walimu wanena
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Neluka, iliyopo jijini Dar es Salaam, Khalidi Abdallah, anasema kuwa kuna unafuu kuwafundisha wasichana kuliko wavulana kwani wavulana wanakuwa na mambo mengi, tofauti na wasichana, ambao ni rahisi kuficha mambo yao na kuchukua muda kukusikiliza hata kama wakati mwingine hawaelewi.

“Wasichana ni wasikivu na waelewa na ikitokea ana tatizo ni rahisi kukufuata kutaka ushauri na wakati mwingine ni rahisi kumsaidia akihitaji msaada,
tofauti na wavulana ambao ni nadra kuuliza jambo baada ya mwalimu kutoka darasani, hata kama hajaelewa,”anasema Abdallah.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda, yeye anaunga mkono kwa asilimia 60 utafiti huo akieleza kuwa mara nyingi wanafunzi wa kike  huwa wasikivu tofauti na wavulana jambo linalowasaidia kufikia malengo yao ya elimu.

Anasema kikubwa zaidi kinachowafanya wawe wasikivu ni hali yao ya kutokujiamini kunakotokana na imani kuwa wao hawawezi, hivyo hujibidisha ili kushindana na wavulana ambao wanajiamini kupita kiasi.

Anataja jambo jingine linachowafanya wafanye vizuri zaidi ni kusifiwa pindi wanapofanya vizuri kwa kuonekana kama wao ni miongoni mwa wasiotegemewa kufanya vizuri kulingana na tabia iliyojengeka kwenye jamii kuwa wao hawawezi.

Wazazi wathibitisha
Jamillah Masanja ambaye ni mama wa watoto watano, watatu ni wa kike na wawili wa kiume, anasema kuwa kwa upande wake ameiona hiyo hasa katika suala la kujisomea kwani mtoto wa kike huwa makini bila kuambiwa tofauti na wa kiume, ambao muda mwingine huwa na mambo yao na ni wabishi.

“Wasichana wangu ni wadogo, mkubwa yupo darasa la saba anayemfuatia yupo darasa la tano, wa mwisho la tatu na  kaka zao mkubwa yupo kidato cha nne, anayemfuata anasoma kidato cha pili.

Kazi niliyo nayo ni kwa hawa wakubwa kwani hawapendi kusoma, walikuwa wakifanya vizuri, lakini sasa hakuna kitu hata natamani niwapeleke kwenye shule za bweni,” anasema mama huyo.
Hata hivyo, Jafari Ibrahimu, baba wa watoto wawili wa kiume anasema kuwa hajakutana na tatizo hilo kwa kuwa watoto wake wapo kwenye shule za bweni, ingawa anapata wasiwasi na matokeo yao.

Anasema walipokuwa watoto wake wako kidato cha kwanza na cha pili walikuwa wakifanya vizuri tofauti na wanavyozidi kupanda wanapunguza juhudi ya kufanya vizuri darasani.

Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) , Joviter Katabalo  anasema kuwa wasichana hupevuka mapema kuliko wavulana, jambo ambalo huwafanya wawe makini zaidi kuliko wavulana.

Anasema wasichana wana uwezo wa kuelewa na kutambua mambo haraka, ingawa kuna baadhi ya tamaduni za Kiafrika zinawanyima uhuru wa kufanya mambo fulani. Matokeo yake wanakosa kujiamini jambo ambalo kwa namna moja au nyingine limewafanya wafanye vizuri wakiamini wanakosea.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger