Mkandarasi Mashauri na msimamizi wa mradi huo, kulia Simon Dohner. |
Kwa ufupi
“Kwa maana hiyo yatakuwa hayachangamani na mabasi mengine ya abiria kwa kuwa yatatumia barabara zake, ndiyo maana yatakuwa yanakwenda kwa kasi ukilinganisha na mengine,” anasema Mhandisi Wambura
ILIANZA kama hadithi ambayo ilikuwa vigumu kueleweka katika masikio ya walio wengi.
Hadithi hiyo ikatungiwa nyimbo zilizoghani mashairi yakizinadi ahadi lukuki zisizoisha za viongozi. Lakini sasa…Ahadi hiyo ipo karibu kutimia.
Mojawapo ni ahadi ya mradi wa mabasi yaendayo kasi ( Bus Rapid Transit-BRT) ambayo kwa sasa inaelekea kutimia kutokana na ujenzi wa kasi unaoendelea katika Barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam.
Ni mradi mkubwa sana ambao pia ni wa kipekee uliotajwa kwa miaka mingi, pengine zaidi ya miaka minane iliyopita.
Ulitajwa lakini bila kudhihirika machoni mwa Watanzania na kusababisha wengi wanung’unike, baadhi yao wakiwamo wanasiasa wakiilaumu Serikali kwa kutoa ahadi hewa.
Hata hivyo, mwanzoni mwa mwaka 2012, mradi huo uliondosha kiu ya Watanzania na shamrashamra za ujenzi zilianza.
Shughuli za ujenzi hazikuwa njema mno hasa kwa wakazi wa maeneo ambayo mradi huo unapita.
Mambo yalibadilika, nyumba zilibomolewa ili kupisha mradi huo, vumbi lilitimka na msongamano wa magari ulikithiri.
Miti mingi iliyozoeleka na wengi kwa kutoa kivuli kando kando ya Barabara ya Morogoro iling’olewa kwa kijiko na kubadilisha kabisa mandhari ya jiji.
Hata hivyo, kwa upande wa pili wa shilingi, ujenzi huo ni mchakato ambao una faida kwa maendeleo ya taifa.
Mradi huo ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia, (WB) utagharimu zaidi ya Shilingi 288 bilioni hadi kukamilika kwake.
Awamu ya kwanza ya mradi - eneo la Kimara
Katika eneo la Kimara, Barabara ya Morogoro, ndipo awamu ya kwanza ya mradi huu ilipoanza kutekelezwa.
Hapa ndipo historia ya Tanzania itakapojengwa kwani madaraja matano ya awali na barabara za mabasi hayo ndipo zitakapopita.
Hata hivyo, madaraja mengine, vituo na barabara za mabasi yaendayo kasi vitaendelea kujengwa jijini Dar es Salaam katika maeneo mengine yakiwamo Morocco, Kamata na Feri.
Pamoja na madaraja hayo matano, barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 20.9, itakuwa na vituo vidogo 29 vya abiria na vituo vikuu vitano.
Mkandarasi wa mradi huo katika eneo la Kimara, Juma Mashauri Wambura amesema mradi huo haumaanishi kuwa mabasi hayo yatakuwa yakitumia umeme, bali yatatumia barabara zake peke yake na kwa maana hiyo hakutakuwa na mwingiliano na magari mengine.
“Kwa maana hiyo yatakuwa hayachangamani na mabasi mengine ya abiria kwa kuwa yatatumia barabara zake, ndiyo maana yatakuwa yanakwenda kwa kasi ukilinganisha na mengine,” anasema Mhandisi Wambura
Mkandarasi huyo anauzungumzia mradi huo na kusema kuwa umegawanyika katika makundi makuu mawili. Nayo ni kazi za ujenzi wa barabara za mabasi hayo na ujenzi wa maumbo au majengo, kama madaraja, vituo vikuu na vidogo.
Anasema mradi huo ambao upo katika hatua ya mwanzo unaendelea kwa kasi kutokana na nguvu iliyowekwa kwa watendaji wote.
“Tunafanya kazi kama timu, watendaji wote tunashirikiana na ndiyo maana unaona sasa mradi unakwenda kwa kasi,” anasema mkandarasi huyo.
Hata hivyo, mkandarasi huyo anasema changamoto kubwa iliyopo ni kwa Serikali kuchukua muda mrefu katika utekelezaji wa baadhi ya mambo, jambo linalokwamisha utendaji.
Anasema na kutoa mfano kuwa nyaya za umeme zilizopo upande wa kushoto wa daraja hilo, ilipo Baa ya Pavinia mpaka sasa hazijaondolewa, kitendo kinachochelewesha ujenzi wa sehemu ya msingi wa daraja.
“Nafikiri Wizara ya Nishati na Madini na wenzao wa Ujenzi wanashindwa kushirikiana katika kutatua tatizo hilo ndiyo maana mpaka sasa, nyaya hizo hazijaondolewa ili kuturuhusu tuendelee na ujenzi,” anasema Wambura.
Pia mkandarasi huyu anasema umbali wa eneo la kituo hicho unaweza kuwa ni kikwazo kwa wakazi wa jiji hilo.
Anasema umbali ndani ya daraja hilo kutoka chini kwenda juu hadi kufika chini katika eneo la kupandia basi , ni sawa na viwanja viwili vya mpira.
“Mtu anaweza kutembea kwa dakika 13 hadi 15 ili kufika katika kituo chake cha kupandia basi, ndani ya daraja hilo. Nahisi inaweza kuwachukua muda mrefu Watanzania kuielewa hali hiyo,” anasema.
Naye msimamizi wa mradi katika eneo hilo, Simon Aigner anasema anapata ushirikiano mzuri kutoka kwa wafanyakazi, raia wa Tanzania.
“Ninapata changamoto kidogo kwa sababu hili ni taifa jipya, utamaduni mpya na watu wapya lakini katika kazi, tunakwenda vyema,” anasema Aigner, ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Strabag kutoka Ujerumani.
Maoni ya wakazi wa Kimara
Baadhi ya wakazi wa Kimara, eneo la kandokando ya Barabara ya Morogoro nao wana mengi ya kusema kuhusu mradi huo.
Kijana anayejishughulisha na kubeba mizigo katika eneo hilo, Andrea Mwakabonga anasema mradi huo hauna mafanikio yoyote kwa vijana wa rika lake ambao walitarajia kupata ajira.
“Wakati mradi unaanza nilitarajia kupata kibarua japo cha kubeba mizigo kama zege, mbao na kadhalika lakini nasikitika kuwa shughuli hii imekuja kwetu bila kutunufaisha,” anasema Mwakabonga.
Anasema licha ya kukosa ajira lakini upanuzi wa barabara hiyo kwa ajili ya mradi huo unazorotesha kazi zao za kubeba mizigo baada ya vituo vingi kubadilishwa.
Mwakabonga anaongeza kuwa mradi huo ulitarajiwa kuwapa ajira watu wa maeneo hayo badala ya kuwalisha vumbi bila hata ya kuwapa kazi ya kujipatia kipato lakini sivyo.
“Tupo tayari kuwajibika, nguvu tunazo lakini tunaambiwa kuwa tukaombe kazi wizarani (Ujenzi), nani anatujua huko,” anasema.
Mwakabonga anaongeza kuwa anafahamu fika kuwa mradi huo una manufaa kiuchumi na utapunguza foleni lakini hauna mafanikio kwa mtu mmoja mmoja hasa asiyetumia usafiri kama yeye.
Sada Juma, ambaye ni mfanyakazi katika Baa ya Pavina iliyoko Kimara Mwisho anasema mradi huo umepoteza mwelekeo kwa wafanyabiashara wengi katika eneo hilo.
Anasema tangu barabara ipanuliwe, eneo kubwa la baa hiyo lilimegwa na kusababisha wateja wao kutokufika kabisa katika baa hiyo.
“Pamoja na eneo la baa hii kuchimbwa lakini Serikali haijatwambia lolote kama tuhame au tuendelee na shughuli zetu,” anasema.
Anasema kwa kuwa baa hiyo ipo katika mwinuko, uchimbaji wa mchanga unaofanywa na wafanyakazi wa Strabag, umetengeneza bonde ambalo linaweza kusababisha ajali mbaya.
Itaendelea wiki ijayo.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !