Machafuko makubwa yametokea leo katika kijiji cha Buseresere Wilayani
Chato Mkoani Geita kati ya waslam na wakristu na kupelekea watu 10 kujeruhiwa
vibaya kwa mapanga huku mchungaji wa kanisa la Pentekoste Assemblies of God
Mathayo Kachila (45) akipoteza maisha kwa kuchinjwa na watu wanaodaiwa ni
waumini wadini ya kiislam kisha mwili wake kutelekezwa kwenye vibanda vya
maduka ambavyo vilikuwa jirani na eneo hilo.
Habari za kuaminika kutoka eneo hilo
la tukio lililotokea majira ya asubuhi zimeeleza kuwa chanzo cha machafuko hayo
ni watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa dini ya kiislam kuvamia bucha lililokuwa
likiwauzia nyama wakristo wa kijiji hicho waliokuwa wamepanga foleni kwa wingi
kusubili huduma hiyo.
Imeelezwa kuwa Wakristu hao walikuwa wamechinja ng'ombe mmoja na mbuzi
wawili eneo la Kanisani kabla ya kuleta nyama hiyo katika bucha hilo lililopo eneo la
Buselesele Sokoni na ndipo walipokumbana na kadhia hiyo ya waislamu.
Tukio hilo lilianza majira ya saa 2
asubuhi muda mfupi baada ya nyama kuwasili katika bucha hilo la wakristu kwa ajili ya kuuzwa jambo
linalodaiwa liliwakera waislam ambao waliivamia bucha hiyo kwa lengo la
kuifunga.
Wakati wakristo wakitafakari uwepo wa waislam kwenye bucha lao
lilipambwa kwa maandishi BWANA YESU ASIFIWE,YESU NI BWANA, ndipo waislam ambao
kwa wakati huo walikuwa wametapakaa mtaani kwa lengo la kuhamasishana
waliongezeka eneo lilipo bucha hilo na kisha kuimwagia nyama iliyokuwa kwenye bucha
hilo vitu vinavyodaiwa kuwa ni sumu.
Kutokana na hali hiyo wakristo walionekana kukerwa na kitendo cha
waislam kuimwagia nyama hiyo vitu hivyo na kisha mapambano yalianza baina ya
wakristu na waislam ambapo mbali na wakristu kutumia mawe waislamu wao
walitumia mapanga na majambia.
Hata hivyo wakati mapambano hayo yakiendelea mchungaji huyo ambaye kwa
sasa ni marehemu alifika eneo la tukio ili kujua kulikoni na ndipo naye
alipojikuta akishambuliwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za kichwa chake na
alifia njiani wakati akikimbizwa katika hospital ya Wilaya ya Geita kwa
matibabu zaidi.
Mbali na mchungaji huyo kupoteza maisha,wengine waliojeruhiwa ni pamoja
na Said Ntahompagaze(45),Sadick Yahaya(40),Yasin Rajab(56),Vicent
Damon(22),wote wakazi wa Buselesele na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la
Ramadhani ambaye yuko mahututi katika wodi namba nane katika hospital ya wilaya
ya Geita.
Hata hivyo watu wengine watano ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja
walitibiwa na kuruhusiwa kutokana na hali zao kuwa nzuri.
Jeshi la polisi Wilayani Chato na Geita lilifika eneo la tukio hilo
majira ya saa 4:30 na kukuta uharibifu mkubwa umekwishafanyika ikiwa ni pamoja
na kukuta duka la Mwenyekiti wa BAKWATA wilaya ya Chato Yusuph Idd linalotumika
kwa biashara ya M-Pesa na vinywaji baridi likiwa linateketea kwa moto uliodaiwa
kuwashwa na waumini wa dini ya kiislam.
Mkuu wa Wilaya ya Chato Ludorick Mpogolo aliyefika eneo la tukio muda
mfupi baada ya polisi kuwasili eneo hilo
mbali na kusikitishwa na kitendo hicho aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati
serikali ikiangalia njia sahihi za kutatua mgogoro huo ambao unakuwa kwa kasi
kila kukicha.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili mkuu wa Mkoa wa Geita
Magalula Said Magalula mbali na kuthibitisha kuwepo kwa tukio hilo, alionyesha
kukerwa na watu ambao wanafurahia vurugu zisizo na msingi na kuonya
kuwashughulikia wale wote watakaobainika ni wachochezi wa masuala ya kidini.
Picha na habari kwa hisani ya GSengo Blog
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !