![]() |
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Mhe. Januari Makamba |
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imeanza mchakato wa
kumiliki Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa asilimia 100 ikiwa ni njia mojawapo ya kufanya mageuzi ya
kibiashara na kuliendesha shirika hilo
kisayansi zaidi ya ilivyo sasa.
Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia Mh. Januari Makamba aliyasema hayo mkoani Dodoma mwanzoni mwa wiki hii wakati akielezea mikakati
mbalimbali inayotaka kuchukuliwa na serikali ili kuweza kulimiliki shirika hilo kwa asilimia 100
badala ya 65 za sasa.
Kwa sasa TTCL inamilikiwa kwa
ubia, serikali ikiwa na asilimia 65 wakati 35 zinamilikiwa na kampuni ya simu
za mikononi ya Airtel.
“Mazungumzo tayari yameshaanza na
dhamira yetu ni kununua aslimia 35 ya hisa zinazomilikiwa na wenzetu ili
serikali iweze kumiliki asilimia 100,” alisema Mh. Makamba.
Alisema katika kufanya mipango ya
kwenda mbele kimaendeleo kupitia shirika hili ni lazima kufanya mchakato wa
kulimiliki kwa asilimia 100 ili serikali iweze kufanya mageuzi kwa utashi wake
kadiri inavyofaa.
Alifafanua kwamba hatua hii ni
Kutokana na changamoto zilizopo za kimuundo, kiungozi na ndio maana serikali
imechukua hatua za kinidhamu miongoni mwa baadhi ya watendaji waliobainika
kutumia madaraka yao
vibaya ikiwa ni pamoja na kufanya ubadhirifu na hivyo kulisababishia shirika
hasara.
“Hii ni moja ya hatua muhimu
katika kuelekea kufanya mageuzi katika shirika hili kongwe hapa nchini,”
alisema.
Alizitaja changamoto nyingine
kuwa ni matatizo ya mtaji, na kusema kuwa ni lazima yashughulikiwe ikiwa ni
pamoja na kwenda na teknolojia mpya na kulifanya shirika lijiwekeze kibiashara
zaidi ya ilivyo sasa.
“Naamini katika kufanya mageuzi
makubwa bodi itachukua nafasi yake kwa maana ya uongozi wa shirika katika
kurekebisha mambo na mapungufu yaliyopo, kwa maana ya kuweka uongozi mpya
utakaoleta mabadiliko ili kulibadilisha liwe shirika kubwa la kisasa linalotengeneza
faida,” alisisitiza.
Alisema kutokana na historia yake
huko nyuma kampuni hii ilipaswa kuwa ndio kampuni inayoongoza kimapato na pia
kwa kutoa huduma nchi nzima kutokana na kuwa ipo kila wilaya katika nchi,
lakini kutokana na changamoto mbalimbali imekuwa ni tofauti na matarajio
yaliyowekwa wakati huo.
Alisisitiza kuwa wakati sasa
umefika kwa shirika kuwa katika mtazamo wa kuwekeza kibiashara zaidi na
ushindani.
“Shirika hili kongwe limeendelea
kubaki kama lilivyo na serikali imeliona hilo,
kinachohitajika ni kuwekeza katika rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na
ushindani wa kibiashara uliopo sasa,” aliongeza.
Alisema mbali na changamoto zote
hizo lakini TTCL imefanikiwa kuunganisha Ofisi za Serikali, mashirika
mbalimbali, Taasisi za kifedha, utangazaji na Taasisi za elimu na hivyo
kuboresha matumizi ya huduma za mtandao wa mawasiliano kupitia Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.
“Kwa mfano huduma za video
conferencing zinawezesha kuendesha mafunzo au mikutano kwa wahusika na hivyo
kuongeza ushiriki, na kupunguza gharama,” alisema.
Akisikiliza kero za wafanyakazi wa kampuni
hiyo hivi karibuni, waziri Makamba aliiagiza bodi ya Wakurugenzi ya TTCL
kumtumia Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa mahesabu ili
kuthibitisha tuhuma za ubadhirifu wa fedha za kampuni hiyo ili hatua za
kisheria wakibainika.
Baadhi ya malalamiko yaliyotolewa
na wafanyakazi hao ni pamoja na uongozi na bodi dhaifu katika ufuatiliaji
mambo, ubadhirifu wa fedha za kampuni pamoja na uhamisho wa wafanyakazi
usofuata taratibu.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !