Waziri Mkuu, Raila Odinga na Naibu wake, Uhuru Kenyatta - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » Waziri Mkuu, Raila Odinga na Naibu wake, Uhuru Kenyatta

Waziri Mkuu, Raila Odinga na Naibu wake, Uhuru Kenyatta

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Thursday, February 21, 2013 | 8:08 PM

Waziri Mkuu, Raila Odinga na Naibu wake, Uhuru Kenyatta 
Na  Mwandishi Wetu, Nairobi  (email the author)
Kwa ufupi

Kwa mujibu wa Consumer Insight, iwapo uchaguzi huo
ungeandaliwa leo, Odinga wa Coalition for Reform and Democracy (Cord) atashinda kwa asilimia 45 ya kura. Kenyatta wa Jubilee Coalition atapata asilimia 43, ilhali Mudavadi atapata asilimia tano ya kura hizo.


TAFITI tatu zimeonyesha kwamba Waziri Mkuu, Raila Odinga na Naibu wake, Uhuru Kenyatta wameendelea kuchuana kwa karibu katika kampeni za kumrithi Rais Mwai Kibaki kwenye Uchaguzi Mkuu wa Machi 4, mwaka huu.

Utafiti uliofadhiliwa na Nation Media Group (NMG) na kuendeshwa kati ya Februari 14 na 17, mwaka huu ulionyesha kwamba Odinga bado yuko mbele, akifuatiwa kwa karibu na Kenyatta. Anayewafuatia kwa mujibu wa utafiti huo ni Musalia Mudavadi ambaye yupo katika Muungano wa Amani.

Kampuni tatu za utafiti, Consumer Insight, Strategic Research and PR na Infotrak Research and Consulting, zilitoa matokeo ya uchunguzi wao huru unaoonyesha kwamba hakuna mgombea kati ya hao wawili anayeweza kujizolea umaarufu kwa zaidi ya nusu ya wapigakura 14.3 milioni waliojiandikisha nchini.

Katiba inahitaji mshindi wa urais kupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa na angalau asilimia 25 ya kura katika kaunti 24 kati ya 47 ili kuongoza nchi.

Kwa mujibu wa Consumer Insight, iwapo uchaguzi huo ungeandaliwa leo, Odinga wa Coalition for Reform and Democracy (Cord) atashinda kwa asilimia 45 ya kura. Kenyatta wa Jubilee Coalition atapata asilimia 43, ilhali Mudavadi atapata asilimia tano ya kura hizo.

Mgombea wa Muungano wa Eagle, Peter Kenneth atapata asilimia tatu, ilhali mgombea wa Narc Kenya, Martha Karua ataambulia asilimia moja ya kura. Asilimia mbili ya wapiga kura bado haijaamua ni nani wa kuungwa mkono.

Kwa upande wake, Strategic Research iligundua kwamba Odinga atamshinda Kenyatta kwa nusu ya asilimia moja. Inabashiri kuwa Odinga atashinda kwa asilimia 44.4 huku Kenyatta akipata asilimia 43.9. Mudavadi, kwa mujibu wa utafiti huo, atapata asilimia 6.4 ya kura, ilhali Kenneth atapata asilimia 2.8 huku Karua akipata asilimia 1.9.

Utafiti wa Strategic Research ulionyesha kuwa hakuna mgombea yeyote, kati ya watatu waliosalia anayeweza kupata zaidi ya asilimia moja ya kura. Ilionyesha kuwa Mohammed Abduba Dida wa Alliance for Real Change atapata asilimia 0.2, Paul Muite wa Safina (asilimia 0.1) na James ole Kiyiapi wa Restore and Build Kenya (asilimia 0.3).

Kadhalika, utafiti wa Infotrak Research and Consulting ulionyesha kuwa Waziri Mkuu Odinga alikuwa mbele. Matokeo ya uchunguzi wake yalionyesha kuwa angeshinda kwa asilimia 45.9 akifuatwa na Kenyatta kwa asilimia 44.4 na Mudavadi kwa asilimia sita na Peter Kenneth kwa asilimia 1.9.

Kimsingi, utafiti wa kampuni hizo tatu umebainisha kwamba huenda Wakenya wakasubiri hadi Aprili kumpata Rais wa Nne kama hakutatokea jambo linaloweza kubadili mwelekeo wa sasa wa kisiasa katika siku hizi chache zilizosalia kuelekea uchaguzi.

Uhuru atangaza kujitoa mdahalo

Katika hatua nyingine, Kenyatta ametangaza kwamba amejitoa kwenye mdahalo wa pili wa wagombea urais. Mdahalo huo umepangwa kufanyika Jumatatu ijayo.
Hatua hiyo ya Kenyatta inatokana na malalamiko yake kwamba hakutendewa haki katika mdahalo wa kwanza wa Februari 11, mwaka huu baada ya waendeshaji wake kuingiza mambo ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai(ICC) dhidi yake.

Timu ya kampeni ya Jubilee imeeleza kwamba kwa kuruhusu mjadala huo, kulitoa nafasi kwa wagombea wengine kutokuguswa kwa kashfa zao za kitaifa zinazowahusu ambazo ilidai kuwa ni kubwa zaidi ya hiyo.

“Tulitegemea kuwa baada ya kutambulishwa katika mjadala wa kwanza na kuhusishwa kwa Kenyatta na ICC vilevile tulitegemea maswali magumu pia yangeulizwa kwa wagombea wengine hasa: “Kashfa ya Maize na Kazi kwa Vijana” inayomhusisha Odinga,” imesema taarifa ya timu hiyo.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger