JK aamuru waliomuua padri wasakwe - Arusha Forum
Headlines News :
Home » » JK aamuru waliomuua padri wasakwe

JK aamuru waliomuua padri wasakwe

Written By Sema Naye - Naipenda Tanzania on Monday, February 18, 2013 | 2:41 AM


 

MAUAJI ya Padri Evaristus Mushi (56) wa Kanisa Katoliki Zanzibar, yamepokewa kwa mshituko na Rais Jakaya Kikwete, ambaye tayari ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike mara moja.

Taarifa ya Ikulu iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa Rais Kikwete ameagiza Polisi nchini kukusanya nguvu zake zote na maarifa yake yote, kufanya uchunguzi huo wa kina na kwa haraka.

“Nimeliagiza Jeshi Polisi nchini, kukusanya nguvu zake zote na maarifa yake yote, kuhakikisha uchunguzi wa kina na wa haraka sana unafanyika, ili kubaini mhusika ama wahusika na kuwakamata, ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria,” alisema Rais Kikwete.

Mbali na Polisi kutakiwa kutumia nguvu na maarifa yote, pia Rais Kikwete ameitaka kuongeza nguvu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama vya ndani na nje ya nchi.

“Nimewaagiza polisi washirikiane na vyombo vingine vya usalama nchini na mashirika ya upelelezi ya nchi rafiki, katika kufanya uchunguzi wa mauaji haya.

“Nataka ukweli wake ujulikane, ili kama kuna jambo lolote zaidi, lishughulikiwe na kukata mzizi wa fitina,” alisema Rais Kikwete.

Wakati hatua hizo zikichukuliwa, Rais Kikwete amewataka waumini wa Kanisa Katoliki na wananchi wote, kuwa watulivu wakati Serikali ikishughulikia suala hilo kwa kuwa hakuna mtu wala watu ama kikundi cha watu, kitachoruhusiwa kuvuruga amani ya nchi yetu.

Rambirambi Wakati huo huo, Rais Kikwete anawapa pole nyingi na rambirambi za dhati ya moyo wake Baba Askofu Augustino Shayo wa Jimbo Katoliki, Zanzibar, maaskofu wote nchini na waumini wote wa Parokia ya Minara Miwili kwa msiba huo mkubwa uliowakuta.

”Napenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja katika kuomboleza kifo cha mpendwa marehemu Padri Evaristus Mushi na kuwa msiba huu ni wa kwetu sote,” alisema Rais Kikwete.

Tayari Polisi imetuma timu ya wataalamu waliobobea kwenye masuala ya intelijensia, upelelezi na operesheni kutoka Makao Makuu ya Polisi. Wataalamu hao wametakiwa kushirikiana na timu ya wataalamu iliyoko Zanzibar, kuchunguza kwa kina matukio hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema, alisema timu hiyo imeundwa na viongozi wa Chuo cha Naibu Kamishna wa Polisi (ACP), Peter Kivuyo, atakayesimamia taarifa za kiintelejensia, Simon Siro, atakayesimamia operesheni na Samson Kassala atakayesimamia upelelezi.

Tayari Polisi inawashikilia watu watatu kwa mahojiano ya awali ambapo IGP Mwema alisema tukio la kuuawa kiongozi wa dini ni baya na la kusikitisha.

“ Kutokana na tukio hili na kujirudia kwa vitendo vya kuwashambulia na kuwadhuru viongozi wa dini na uchomaji wa nyumba za ibada, Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, tumeanza uchunguzi wa kina wa kuafuatilia wanaohusika na matukio hayo,” alisema.

IGP Mwema pamoja na kuwaomba wananchi kuwa watulivu, pia aliwaomba watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa za kusaidia kukamatwa wahalifu hao, kwa kupiga simu za makamanda wa mikoa na vikosi mbalimbali vya Jeshi hilo.

“Polisi inahitaji sana ushirikiano wa wananchi, kama ambavyo wananchi walinisaidia katika operesheni ya kupambana na majambazi waliokuwa wanavamia mabenki, ushirikiano wa wananchi unahitajika sana kwa sasa,” alisema.

Alisema Polisi imeimarisha doria maeneo yote nchini na kufuatilia mienendo na kuwakamata watu wote wanaochochea, kufadhili, kuhamasisha na kushiriki katika vitendo vya uhalifu, vurugu na fujo.

Zanzibar walaani Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na CCM, wameshutumu mauaji hayo na kuonya kwamba yanahatarisha amani na utulivu uliopo sasa. Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi ambaye alikuwepo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja akiwa na waumini wengine wa dini ya Kikristo, alielezea kusikitishwa na mauaji hayo.

“Nimesikitishwa na tukio hili ambalo ni la pili linalowahusisha viongozi wa dini ya Kikristo… nasisitiza suala la amani na utulivu na watu kuacha kuchukua sheria mikononi mwao,” alisema.

Mbunge wa Dole, Silvester Mabumba, alisema kuna watu wenye nia ya kutaka kuharibu utulivu wa nchi, wanaofanya hujuma kwa viongozi wa dini.

Imeandikwa na Anastazia Anyimike, Dar na Khatib Suleiman, Zanzibar
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Arusha Forum - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger