MHESHIMIWA MIZENGO P.
PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
|
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, tumekuwepo hapa
Bungeni, Dodoma
kwa takriban siku 11 ambapo leo tunahitimisha shughuli zilizopangwa katika
Mkutano wa Kumi wa Bunge lako Tukufu. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi
Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote
naomba nitumie nafasi hii kutoa pole kwa Ndugu, Jamaa na Marafiki waliopoteza
Wapendwa wao katika ajali mbalimbali zilizotokea hapa Nchini, ikiwemo ajali ya
Jahazi la Sunrise
iliyotokea Wangwi katika Bahari ya Hindi na Ajali ya Lori kule Mbarali ambapo
Watu wamepoteza maisha na kupata majeraha. Aidha, tunawapa pole Majeruhi wote
na Abiria waliopoteza mali
katika ajali hizo. Kwa kipekee kabisa napenda kutoa pole kwa Ndugu, Jamaa na
Marafiki wa Askofu Thomas Laiser wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati - Arusha
ambaye amefariki jana Mchana na Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Kanisa Katoliki,
Jimbo la Moshi ambaye amefariki Usiku wa
kuamkia leo huko Nairobi alikokuwa anapata matibabu. Wote tunawapa pole sana!
SHUGHULI ZA BUNGE
a) Maswali
3. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano
huu jumla ya Maswali 116 ya Msingi na 286 ya nyongeza yalipatiwa majibu.
Vilevile, Maswali 6 yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa
Papo kwa Waziri Mkuu.
b) Miswada
4. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano
huu, Miswada ifuatayo ilisomwa kwa mara ya Kwanza:
i) Muswada wa Sheria ya Vyama vya
Ushirika wa Mwaka 2013 [The Cooperative Societies Bill, 2013]; na
ii) Muswada wa Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali wa Mwaka 2013 [The Written Laws Miscellaneous Amendments, Bill
2013].
5. Mheshimiwa Spika, Muswada wa
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2012 [The Written Laws Miscellaneous
Ammendments (No. 3) Act, 2012] ulisomwa kwa mara ya Pili na kupitia ngazi zake
zote;
c) Hoja Binafsi za Wabunge
6. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano
huu, pia Waheshimiwa Wabunge walipata
fursa ya kuwasilisha Hoja Binafsi kama
ifuatavyo:
i) Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Mwigulu
Lameck Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi ya kuitaka Serikali iwasilishe
Bungeni Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Mfuko wa Elimu ya Juu (The Higher
Education Fund Act);
ii) Hoja Binafsi ya Mheshimiwa James
Francis Mbatia, Mbunge wa Kuteuliwa kuhusu udhaifu ulioko katika Sekta ya Elimu
Nchini;
iii) Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Dkt.
Hamisi Andrea Kigwangalla, Mbunge wa Nzega ya kuitaka Serikali ianzishe Mpango
Maalum wa Kukuza Ajira kwa Vijana na kuanzisha Mfuko wa Mikopo ya Vyama
Wanaowekeza kwenye Kilimo na Viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja na
Kilimo; na
iv) Hoja Binafsi ya Mheshimiwa John
Mnyika, Mbunge wa Ubungo juu ya Kuboresha Upatikanaji wa Maji Safi na ushughulikiaji
wa Maji Taka katika Jiji la Dar es
Salaam.
d) Maazimio
7. Mheshimiwa Spika, vilevile, katika
Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kujadili na kupitisha Maazimio Mawili
yafuatayo:
i) Azimio la Bunge la Kujiunga na Mkataba
wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu Dhidi ya Watu wenye Kinga ya Kimataifa pamoja na
Wakala wa Ki-Diplomasia (Convention on The Prevention and Punishment of Crimes
Against Internationally Protected Persons Including Diplomatic Agents 1973); na
ii) Azimio la Bunge la Kujiunga na Mkataba wa
Kimataifa wa Kuzuia Vitendo vya Ugaidi wa Kutumia Nyuklia (International
Convention for Suppression of Act
of Neuclear Terrorism, 2009).
Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge
kwa kukamilisha Mijadala hiyo.
UJENZI WA UMOJA WA KITAIFA
8. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya
pekee Taifa letu limejaliwa na Mwenyezi Mungu kutimiza miaka zaidi ya 51
sasa ya Uhuru likiwa bado linaendelea
kudumisha Umoja wa Kitaifa. Umoja
huu wa Kitaifa umejengwa kwenye nguzo na misingi imara ya Amani, Utulivu
na Mshikamano. Mimi naamini sote tunapaswa kujivunia Umoja huu wa Kitaifa ambao
ni Tunu kubwa na nguzo muhimu ya maendeleo yetu. Msingi mkubwa wa Umoja wa
Kitaifa tunaoshuhudia leo uliwekwa na malezi mazuri ya Waasisi wa Taifa hili
wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid
Amani Karume. Aidha, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inasisitiza, pamoja na mambo mengine, kujenga Jamii inayozingatia misingi ya
Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Ni jukumu la kila Mwananchi kulinda Umoja huu
ambao hauna mbadala.
9. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu ina
Makabila zaidi ya 120 ambayo kwa Mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi
ya Mwaka 2012 yamefikisha Idadi ya Watu Milioni 44.929. Aidha, hivi sasa tuna
Madhehebu ya Dini yaliyoandikishwa takriban 885 na Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali zaidi ya 6,675 na tumejenga Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa
ambapo hadi sasa tuna Vyama vya Siasa 19 ambavyo vimepata Usajili wa Kudumu.
Licha ya kuwepo kwa Idadi kubwa ya Watu wa Makabila tofauti yenye desturi
mbalimbali na makundi mbalimbali ya Madhehebu ya Dini, Itikadi za Kisiasa na
Watu wenye Rangi mbalimbali, bado tunajivunia kwamba tunaheshimiana na
hatubaguani kwa namna yoyote ile. Hali hii ya amani imeipatia Nchi yetu sifa
Kitaifa na Kimataifa na mfano wa kuigwa.
10. Kutokana na Demokrasi pana iliyopo,
Wananchi wetu wana Uhuru mkubwa wa kutoa maoni, kuanzisha na kujiunga na Vyama
vya Siasa pamoja na kushiriki katika kuchagua Viongozi wa Chama chochote
wanachokipenda kwa kuzingatia Misingi ya Katiba na Sheria za Nchi. Vilevile,
Serikali imetoa uhuru mkubwa wa kupata na kutoa habari kwa uwazi bila vikwazo
vyovyote kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni mbalimbali na Maadili ya
Vyombo vya Habari. Kutokana na Uhuru huo, Idadi ya Vyombo vya Habari
imeongezeka sana
ambapo hadi sasa Idadi ya Vituo 86 vya Redio vilivyopewa Leseni na
vinafanyakazi, Vituo vya Televisheni 26 na Magazeti 768 yaliyoandikishwa na
yanayotolewa na Taasisi mbalimbali.
11. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio
hayo yanayodhihirika wazi, hivi karibuni kumekuwepo na dalili za kupoteza sifa
yetu nzuri ya Umoja wa Kitaifa na Amani ambayo imedumu kwa miaka mingi.
Tumeshuhudia Wananchi mmoja mmoja wakishindwa kuvumiliana, japo kwa tatizo dogo
tu miongoni mwao. Aidha, tumeshuhudia Vyama vya Siasa vikionesha dalili ya
kuhamasisha Wanachama wao kuingia kwenye
malumbano ya Siasa
baina yao wenyewe
kwa wenyewe au baina ya Chama
kimoja cha Siasa na Chama kingine. Baadhi ya Wanachama wameshikana mashati na
kujeruhiana.
12. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia
fursa hii kuwaasa Viongozi wa Vyama vya Siasa kuepuka kutumia majukwaa ya Siasa
kuvuruga Amani yetu na Utulivu uliopo. Waepuke matamko ya vitisho na kuhamasisha
Wanachama wao kuendeleza vitendo vya uvunjifu wa amani na kujenga chuki na
uhasama miongoni mwa Jamii na kwa Serikali halali iliyopo madarakani. Pamoja na kutofautiana kwa mawazo na Sera za
Vyama vya Siasa, ni muhimu tujenge mazingira ya kuvumiliana kwa hali ya juu
katika kujenga Demokrasia ya kweli hapa Nchini. Viongozi wa Vyama wanatakiwa
kueleza Sera zao badala ya kutukanana, kubezana, kushutumiana na kuzomeana.
Tujenge Nchi yetu kwa Amani na Utulivu ndipo tutapata maendeleo endelevu.
13. Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia pia
kuibuka kwa choko choko za Kidini. Baadhi ya Waumini wa Dini wamekuwa
wakikashifu Dini nyingine kwa kejeli na vitendo vingine visivyostahili. Aidha,
baadhi ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini wamekuwa wakiwaingiza Waumini wao katika
Migogoro isiyoisha, ikiwa ni pamoja na kufungiana milango na kuzuia Waumini
Wasiabudu siku za Ibada. Napenda kusisitiza kuwa Madhehebu ya Dini yana nafasi
kubwa ya kujenga Umoja wa Kitaifa, Amani na mshikamano. Nawaomba Viongozi wa
Madhehebu ya Dini kutatua kwa amani migogoro iliyopo na kuelimisha Waumini wao
kuthamini, kujenga na kuenzi Amani na Utulivu uliopo Nchini. Serikali imetoa
uhuru wa Wananchi wake Kuabudu, kila mtu kwa Dini anayoitaka. Hivyo, hakuna
sababu ya Dini moja kukashifu Dini nyingine. Aidha, tupinge kwa nguvu zetu zote
choko choko za Kidini ambazo zimeanza kujitokeza katika sehemu mbalimbali
Nchini.
14. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali baadhi yao
yamekuwa yakihusishwa kuwa mstari wa mbele katika kuwarubuni Wananchi kufanya
vurugu zinazolenga kuleta uvunjifu wa Amani. Napenda kusisitiza kuwa Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali yana jukumu kubwa la kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa
kujenga Umoja wa Kitaifa. Viongozi wa Mashirika haya waepuke kutumiwa na baadhi
ya Viongozi kujenga mbegu mbaya kwa Wananchi kuvuruga Amani.
15. Mheshimiwa Spika, nigusie pia Vyombo
vya Habari, ambapo kumekuwa na kutiliana mashaka kwa baadhi ya Vyombo hivyo
kuandika habari za Uchochezi, hivyo kuashiria Uvunjifu wa Amani na Mshikamano
wa Kitaifa tuliojijengea. Vyombo vya Habari vina wajibu mkubwa wa kuelimisha
Umma na kuhabarisha kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo, kama wafanyavyo
wenzetu jirani, husan Vyombo vya Habari vya Nchi ya Rwanda. Aidha, Vyombo hivi vina
fursa nzuri ya kutumia uhuru uliopo kudumisha Amani na Utulivu Nchini.
Tufanye Nini
16. Mheshimiwa Spika, kutokana na
changamoto zilizopo za baadhi ya Watu waotaka kubomoa Umoja wa Taifa letu na
kuhatarisha Amani na Utulivu Nchini, sisi kama
Taifa hatuna budi kufanya yafuatayo:
i) Serikali, Wananchi na Wadau wote
ikiwemo Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini, Vyombo vya Habari, Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali, n.k. tunapaswa tukae chini tuzungumze na kutafakari kuhusu hali
hii;
ii) Tunapaswa kwa namna zote
tuvumiliane na kuheshimiana kwa kuzingatia Utamaduni wa Kitanzania na Misingi
ya Amani na Utulivu tuliojijengea kwa muda mrefu; na
iii) Wananchi wote tuzingatie na
kuheshimu Utawala Bora wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
17. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia
fursa hii kuwaomba sana Wananchi na Watanzania wenzangu kuendeleza umoja
na mshikamano wa Kitaifa ili kudumisha Amani na Utulivu
uliopo Nchini. Ni vyema kutambua kuwa
Amani na Utulivu uliopo Nchini ni
mazingira wezeshi ya kusaidia kila mmoja
wetu kufanya shughuli zake za kijamii na kiuchumi na kujiletea maendeleo. Bila Amani na Utulivu hakuna maendeleo ya
Watu. Kwa upande wa Serikali itahakikisha kwamba, Umoja tuliojijengea
unadumishwa. Taasisi mbalimbali za Serikali, zikiwemo Vyombo vya Dola ni lazima
zihakikishe kwamba, Wananchi wanaishi kwa Amani na Utulivu. Vilevile,
kuhakikisha kuwa, Umoja wa Kitaifa tulioujenga kwa miaka mingi haupotei.
Naziomba Taasisi zote zinazohusika na kusimamia Amani na Usalama kuhakikisha
kuwa, pamoja na Changamoto zilizopo, Umoja wa Kitaifa unadumishwa.
HALI YA CHAKULA NCHINI
i) Hali ya Mazao na Mvua
18. Mheshimiwa Spika, tathmini
iliyofanyika hivi karibuni juu ya upatikanaji wa chakula Nchini na athari za
mvua zinazoendelea kunyesha, inaonesha kuwa maeneo mengi hasa, yale yanayopata
mvua za msimu kama vile Mbeya, Ruvuma, Rukwa,
Iringa, Tabora, na Mtwara mazao mengi yapo katika hatua mbalimbali za ukuaji.
Inatarajiwa kwamba, endapo mvua hizi zitaendelea vema, upatikanaji wa chakula
katika maeneo hayo utakuwa mzuri.
19. Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo
ya hewa, tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi
Januari 2013 inaonesha upungufu wa chakula katika Wilaya 47 zilizoko katika
Mikoa 15 ambazo zitahitaji msaada wa chakula katika vipindi tofauti.
Inakadiriwa kuwa jumla ya Watu 1,615,445 watahitaji jumla ya Tani 32,870 za
chakula.
ii) Hatua Zinazochukuliwa na Serikali
20. Mheshimiwa Spika, kutokana na
matarajio hayo ya uhaba wa Chakula, Serikali itahakikisha kuwa Kitengo cha
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kinaendelea kusambaza mahindi katika maeneo
yenye uhaba wa chakula. Hadi sasa jumla ya Tani 20,000 zilishatolewa kwa Mikoa
ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Morogoro, Lindi, Tanga,
Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na Tabora. Aidha,
Kitengo hicho (NFRA) kitaendelea kununua nafaka mapema baada ya mavuno ili
kuhakikisha kuwa Serikali ina hifadhi ya kutosha ya chakula kwa ajili ya
kusambaza katika maeneo yatakayokuwa na uhaba wa chakula. Hadi tarehe 6
Februari 2013 Ghala la Taifa la Chakula lilikuwa na jumla ya Tani 68,712.9 za
mahindi pamoja na Tani 3,335.989 za Mtama.
21. Serikali itaendelea kufuatilia kwa
karibu hali ya upatikanaji wa
chakula Nchini na kuhakikisha kuwa hakuna Mwananchi
atakayepoteza maisha kutokana na njaa. Nitoe wito kwa Wananchi kuendelea kuweka
utaratibu wa kuhifadhi sehemu ya mavuno yao
baada ya kuvuna kwa ajili ya akiba ya baadaye badala ya kuuza mavuno yao yote.
MAPAMBANO DHIDI YA UGONJWA WA
MALARIA NCHINI
i) Hali Halisi ya Ugonjwa wa
Malaria Nchini
22. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu inayo
changamoto kubwa ya kukabiliana na Magonjwa makubwa Duniani, yakiwemo Malaria,
Kifua Kikuu, UKIMWI, Saratani, n.k. Niruhusu leo katika Hotuba yangu nizungumzie
kidogo kuhusu Ugonjwa wa Malaria. Ugonjwa wa Malaria bado unaongoza kuwa sababu
kubwa za Wagonjwa wengi wanaohudhuria katika Vituo vya huduma za Afya Nchini.
Aidha, ugonjwa huu unaongoza kwa kusababisha vifo, hasa kwa Watoto walio chini
ya umri wa miaka Mitano. Takwimu kutoka Vituo vya kutolea huduma ya Afya Nchini
zinaonesha kuwa, takriban Wagonjwa Milioni 11 hadi 12 huhudhuria katika Vituo
vya huduma za Afya kwa sababu ya ugonjwa wa Malaria. Vilevile, tafiti
zilizofanyika katika Jamii [Tanzania HIV/Malaria Indicator Survey (THMIS)
2011/2012] zinaonesha kuwa Asilimia 10 ya Watoto katika Kaya wana maambukizi ya
vimelea vya ugonjwa wa Malaria.
ii) Jitihada za Serikali katika kumaliza
tatizo la Malaria Nchini
23. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na
tatizo hili katika kuhakikisha Wananchi wanaendelea kujikinga na maambukizi
dhidi ya ugonjwa wa Malaria, Serikali imefanya mambo muhimu yafuatayo:
Moja: Kutekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa
Mapambano Dhidi ya Ugonjwa wa Malaria wa Miaka Mitano (2008-2013) ambao una
lengo la kupunguza vifo kwa Asilimia 80 ifikapo mwaka 2013 mwishoni.
Utekelezaji wa Mpango huu unafanyika kwa kushirikiana na Mikoa, Wilaya na Wadau
mbalimbali hadi katika ngazi ya Jamii;
Pili: Kusambaza na kuongeza matumizi ya
vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu katika Kaya. Hadi sasa zaidi ya
vyandarua Milioni 26 vimesambazwa kupitia Kampeni iliyolenga Watoto wenye umri
chini ya miaka Mitano;
Tatu: Kutekeleza Mpango wa Hati Punguzo
unaolenga kuhakikisha Akina Mama Wajawazito na Watoto wanaozaliwa wanaendelea
kupata vyandarua hivyo na kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Malaria;
Nne: Kuendeleza Mpango wa kunyunyizia dawa
ya ukoko majumbani ili kutokomeza mazalia ya Mbu. Mpango huo unaendelea kutekelezwa
katika Mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara ambapo zaidi ya Kaya 1,440,000 sawa na
Asilimia 90 katika Wilaya za Mikoa hiyo zitanyunyiziwa viuatilifu. Kutokana na
Mpango huo, zaidi ya Watu 6,500,000 wameendelea kukingwa dhidi ya maambukizi ya
ugonjwa wa Malaria;
Tano: Kuendeleza Mpango wa kuangamiza
viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia njia za Kibaiolojia. Mpango huu ambao unafanywa
na Serikali kwa ushirikiano na Serikali ya Nchi ya Cuba
unatekelezwa katika Jiji la Dar es
Salaam kuanzia mwaka 2011;
Sita: Kutumia Mwongozo wa kutibu ugonjwa wa
Malaria isiyo kali kwa kutumia Dawa ya Mseto ya Artemether/Lumefantrine (ALu).
Mwongozo huu unaendelea kutumika katika Vituo vyote vya Umma vya kutolea huduma
za Afya; na
Saba: Kusambaza kipimo cha haraka cha kutambua
na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya Malaria kwenye damu katika Vituo vyote vya
Umma vya kutoa huduma za afya Nchini.
iii) Changamoto
24. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio
hayo makubwa yaliyopatikana, bado kuna changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa
kazi. Changamoto hizo ni pamoja na:
Moja: Kujitokeza kwa usugu wa mbu dhidi ya
viuatilifu vya aina ya “pyrethroids” vinavyotumika katika vyandarua na
unyuziaji dawa ya ukoko majumbani;
Pili: Kupata vyanzo zaidi vya fedha za
ndani za kuendeleza mkakati wa unyunyiziaji dawa ya ukoko majumbani;
Tatu: Uwezo mdogo wa uzalishaji wa dawa za
kuangamiza viluwiluwi vya Mbu na kuanza kuangamiza Viluwiluwi hivyo katika Jiji
la Dar es Salaam;
na
Nne: Kuendeleza uhamasishaji Wananchi
kutumia nyenzo na kushiriki katika mikakati iliyopo, hasa inayohitaji ushiriki
wao wa moja kwa moja, kama kuharibu mazalia ya
Mbu.
iv) Matarajio ya Mkutano wa United Against
Malaria – Afrika Kusini
25. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za
kupambana na Malaria Duniani, Shirika la Roll Back Malaria Partnership
wakishirikiana na Wizara ya Afya ya Afrika Kusini wanatarajia kufanya Mkutano
mkubwa unaohusu mapambano dhidi ya Malaria kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) kuanzia tarehe 9 - 11 Februari, 2013. Mkutano huo
unatarajia kukutanisha Viongozi wa ngazi ya juu kutoka Nchi za SADC ikiwa ni
pamoja na baadhi
ya Marais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri wa
Afya na Mawaziri wa Michezo katika Nchi hizo. Mkutano
huo pia utajumuisha Viongozi wa juu wa Makampuni mbalimbali ya Sekta Binafsi.
26. Mheshimiwa Spika, lengo la Mkutano huo
ni kukutanisha Viongozi mbalimbali kwa lengo la kuendesha mjadala kuhusu janga
la Malaria katika Nchi za Afrika; ikizingatiwa kuwa ufadhili wa utekelezaji wa
mikakati mbalimbali unazidi kupungua. Mkutano huo unategemewa kuwa chachu kwa
Viongozi kuongeza Bajeti za udhibiti wa Malaria Nchini mwao na kuongeza
ushirikiano na Sekta Binafsi pamoja na Sekta ya Michezo, hususan katika Mpira
wa Miguu katika dhana nzima ya Mpango wa “Safe Companies”. Aidha, Mkutano huo
unatarajiwa kuongeza kasi ya Kupambana dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika Nchi
hizo.
27. Ni matumaini yangu kuwa, Mkutano huo
utakuwa wa mafanikio makubwa kwa Nchi za Kusini mwa Afrika katika vita dhidi ya
ugonjwa wa Malaria. Vilevile, utatupatia uzoefu kwa Nchi yetu katika kupambana
na Ugonjwa huu wa Malaria.
v) Jitihada za Chama cha Wabunge cha
Kupambana na Malaria
28. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za
kupambana na Malaria Nchini, Muungano wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania
walianzisha Asasi inayojulikana kama Tanzania
Parliamentary Against Malaria (TAPAMA). Lengo la kuanzishwa kwa Asasi hii ni
kuongeza utashi wa Kisiasa katika kushiriki na kutekeleza Mpango na Sera ya Taifa ya kutokomeza Ugonjwa
wa Malaria Nchini. Asasi hii ilisajiliwa mwaka 2008 na hadi sasa imetekeleza
masuala mbalimbali katika jitihada zake za kupambana na Malaria Nchini kama
ifuatavyo:
Moja: Ugawaji wa Vyandarua kwa Watoto
wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa Mikoa ya Ruvuma,
Kilimanjaro na Mwanza ambapo zaidi ya Watoto 2,500 walifaidika na huduma hii;
Pili: Kufanya mazungumzo na Wawakilishi wa
Bunge la Jumuiya ya Ulaya mwaka 2009 waliotembelea Tanzania
na kuona uwezekano wa Jumuiya ya Ulaya kusaidia zaidi Mapambano dhidi ya
Malaria Tanzania.
Aidha, walifanya mazungumzo na Viongozi na Wawakilishi wa Asasi ya Malaria No
More ya Marekani, ambao waliongozwa na Balozi Mark Green na kuwezesha kuanza
kwa Mradi wa Zinduka, Malaria Haikubaliki;
Tatu: Kushiriki Kikao cha Nchi za Jumuiya ya Ulaya Nchini
Ufaransa mwaka 2009 ili kujadili juhudi za Viongozi wa Kisiasa katika
Kupamabana na Malaria Nchini;
Nne: Kushiriki kutayarisha Mwongozo
(Advocacy Guideline) utakaotumiwa na Wabunge, Madiwani na Viongozi wengine wa
Kisiasa na Kijamii katika Utekelezaji na ushawishi wao katika kutokomeza
Malaria Tanzania.
29. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii
kuwapongeza Wajumbe wote wa TAPAMA chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Riziki Said
Lulida, Mbunge wa Viti Maalum kwa juhudi zao za kuhakikisha kuwa wanaungana na
Wadau wengine Nchini na Duniani katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria.
Nazipongeza pia Taasisi Zisizo za Kiserikali kwa ujumla wao ambazo zimejitokeza
katika Mapambano dhidi ya Magonjwa mbalimbali, yakiwemo UKIMWI, Kifua Kikuu,
Saratani, n.k. Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge zaidi wazidi kujiunga na Asasi
hizi na hasa za Magonwa ili kuweka hamasa kwa Wananchi katika Kupambana na
Maradhi hayo. Aidha, natoa wito kwa Wananchi wote kwa ujumla kuunganisha nguvu
za Kupambana na Ugonjwa huu wa Malaria ili kunusuru nguvukazi ya Watanzania.
Suala kubwa ni kuzingatia masharti ya Wataalam kuanzia katika kutunza mazingira
yetu na kutumia Vyandarua kama kinga iliyo ya
uhakika.
LISHE
30. Mheshimiwa Spika, wakati nikitoa hoja
ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge,
mwezi Novemba, 2012 nilieleza kwa kifupi utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa
Lishe wa Mwaka 2011/2012 – 2015/2016. Pamoja na mambo mengine nilionesha hatua
ambazo Serikali inachukua
kuondokana na tatizo
la Lishe Nchini.
Jambo kubwa na la msingi katika kupambana na tatizo la Lishe ni kutoa
elimu kwa Jamii ili kula vyakula vyenye Virutubisho muhimu hasa kwa Mama
Wajawazito na Watoto Wachanga. Jitihada za Serikali za kuwashirikisha Wadau
mbalimbali katika kutoa Elimu ya Lishe Nchini zimeleta mwamko mzuri ambapo
Wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
na Wadau wa Maendeleo sasa wanashiriki kikamilifu katika utoaji elimu na kukuza
kilimo cha mazao yenye virutubisho muhimu ili kuongeza vyakula vyenye
virutubisho.
31. Mheshimiwa Spika, katika kuunga
mkono jitihada za Serikali za kupambana na tatizo la Lishe Nchini, hivi
karibuni Waheshimiwa Wabunge chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Lediana Mafuru
Mng’ong’o Mbunge wa Viti Maalum wameunda Kikundi cha kuongeza hamasa na
kuzidisha chachu ya kutoa elimu kuhusu Lishe Bora hapa Nchini. Nimearifiwa
kwamba, Kikundi hicho cha Wabunge kimekutana tarehe 10 hadi 12 Januari, 2013 na
kukubaliana kuhusu kazi ambazo watafanya ili kuongeza sauti yao kwenye jamii
juu ya umuhimu wa Lishe Bora. Kikundi
pia kimeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitatu (2013-2015) wenye malengo ya
kukuza uelewa wa Umma juu ya Lishe, Chakula na Haki za Watoto. Aidha, kikundi
hicho kiliazimia kushawishi uwekaji wa vipaumbele vya Lishe katika Mipango ya
Maendeleo na Bajeti za Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na
kuingiza masuala ya Lishe, Chakula na Haki za Watoto katika Sera na Mikakati
mbalimbali ya Serikali. Azimio lingine ni kuimarisha usimamizi wa kazi za Bunge
kuhusu Lishe, Chakula na Haki za Watoto.
32. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua
fursa hii kukishukuru kwa dhati kikundi hiki ambacho kimeona umuhimu wa kuunga
mkono juhudi za Serikali za kupambana na tatizo la Lishe, ikiwemo Utapiamlo.
Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuanzisha kikundi hiki.
Niwashukuru kwa kuona umuhimu wa kusimamia tatizo hilo ili kupata suluhu ya kudumu. Ninatambua
pia umuhimu wa Waheshimiwa Wabunge kuhamasisha masuala ya Lishe kwa Wananchi wa
Majimbo yao.
Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wengine wote kushiriki kutoa msukumo wa pekee kwa
Wananchi wa Majimbo yenu katika Mapambano dhidi ya Utapiamlo ili kwa pamoja
tujenge Taifa lenye Watu walio na Lishe Bora. Lengo ni kuwawezesha kuchangia
zaidi katika uzalishaji mali
na ukuaji wa uchumi wa Nchi kwa ujumla.
MCHAKATO KUELEKEA KATIBA MPYA
33. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge
watakumbuka kuwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetangaza kumaliza kazi ya
kukusanya maoni binafsi ya Wananchi mmoja mmoja kama
mchango wao kwa ajili ya kuandika Katiba Mpya. Aidha, imekamilisha kazi ya
kukutana na Makundi Maalum, Viongozi wa Kitaifa Wastaafu na Viongozi wa Kitaifa
waliopo Madarakani. Kwa maana hiyo, Tume sasa imekamilisha kazi ya ukusanyaji
maoni kama ilivyopangwa. Hivi sasa Tume
inaendelea na kazi za uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na Wananchi na yale
yaliyotolewa na Makundi Maalum ili baadaye kutayarisha Rasimu ya Katiba ambayo itawasilishwa katika
Mabaraza ya Katiba yatakayoitishwa na Tume Nchini kote.
34. Kulingana na Ratiba, Mikutano ya Mabaraza
ya Katiba itafanyika kuanzia mwezi Juni, 2013 na itajumuisha Wajumbe
watakaochaguliwa na Wananchi wenyewe kuanzia ngazi ya Kijiji. Wajumbe hao ndio
watapaswa kuwasilisha maoni ya Wananchi katika Mikutano ya Mabaraza.
35. Mheshimiwa Spika, nimearifiwa kuwa
Tume imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa namna bora na ya Kidemokrasia ya kuwapata
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ambao unaendelea kusambazwa Nchi nzima. Mwogozo
huo tayari umetangazwa katika Vyombo vya Habari ili Wananchi waufahamu na kutoa
maoni kuhusu namna ya kuuboresha.
36. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Rasimu
hiyo ya Mwongozo, katika Mikoa ya Tanzania Bara ukiondoa Mkoa wa Dar es Salaam,
kila Kata itawakilishwa na Wajumbe wanne (4) watakaochaguliwa kutoka miongoni
mwa Wakazi wa Vijiji vilivyopo kwenye Kata ambao wataungana na Madiwani wa Kata
na Madiwani wa Viti Maalum kuunda Baraza la Katiba la Wilaya. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Tume
imeandaa utaratibu tofauti wa kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
ambapo kila Kata watatoka Wajumbe wanane (8) ambao wataungana na Madiwani wa
Kata na Madiwani wa Viti Maalum. Kwa
msingi huo, kutakuwa na jumla ya Wajumbe 18,169 watakaohudhuria Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya Kwa Tanzania Bara.
37. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar, kutakuwa na
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa 13. Kila Shehia itawakilishwa na Wajumbe watatu
(3), ambao wataungana na Madiwani wa Wadi, Madiwani wa Viti Maalum na Madiwani
wa kuteuliwa waliopo kazini kwa sasa. Kwa msingi huo, Wajumbe wote wa Mabaraza
ya Katiba kwa Zanzibar
watakuwa 1,198.
38. Wananchi wanaopenda kuwa Wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya watatakiwa kuwasilisha majina yao kwa Maafisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa
upande wa Tanzania Zanzibar watawasilisha kwa Sheha kwa tarehe itakayoelekezwa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba hapo baadaye.
39. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito
kwa Viongozi wote katika ngazi za Wilaya na Serikali za Mitaa kusimamia
kikamilifu utaratibu ambao umewekwa na Tume. Kwa kufanya hivyo, Wajumbe ambao
watashiriki katika Mabaraza ya Katiba
watapatikana kwa njia za Kidemokrasia na hivyo, kufanikisha Vikao vya Mabaraza ya Katiba. Ni
matumaini yangu kuwa Wananchi watausoma Mwongozo huo, na baadaye kuwasilisha
mapendekezo na maoni yao
kwa Tume kabla ya kazi ya uchaguzi wa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanza
rasmi.
40. Nitumie fursa hii kuwaomba Wananchi
wote kushiriki kikamilifu kutoa maoni kuhusu Mwongozo huo na pia katika kuwapata
Wajumbe watakaoshiriki katika Mabaraza ya Katiba kwa mujibu wa Sheria, na
vilevile Wajumbe hao washiriki kikamilifu katika Vikao vya Mabaraza ya Katiba
na kutoa maoni kwenye Rasimu ya Katiba.
RIPOTI YA TATHMINI YA UTAWALA
BORA AFRIKA (APRM)
41. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza dhamira
ya uwazi na ujenzi wa pamoja wa utawala bora nchini kwa kuwashirikisha
Wananchi, Nchi yetu imekuwa miongoni mwa Nchi 33 za Umoja wa Afrika zilizoamua
kwa hiari yake kujiunga na Mpango wa Bara la Afrika wa Kujitathmini Kiutawala
Bora (The African Peer Review Mechanism - APRM). Tanzania ilijiunga na mchakato huo
mwaka 2004, na Bunge liliuridhia mwaka
2005.
42. Mheshimiwa Spika, Mpango huu wa
kujithamini Kiutawala Bora ni muhimu kwetu na unaakisi Sera zetu na za Waasisi
wa Taifa hili juu ya Kujikosoa na Kujisahihisha. Aidha, unahusisha Viongozi wa
Afrika na unatoa fursa kwa Wananchi kutathmini hali ya Utawala Bora katika Nchi
zao na kuainisha kwa pamoja mambo mazuri yanayopaswa kuendelezwa na yale yenye
changamoto za kufanyiwa kazi. Miongoni mwa sababu za Nchi yetu kujiunga na
Mpango huu ni kutokana na ukweli kwamba Watanzania tuna mengi ya kuifundisha
Afrika na Watu wake kuhusu Utawala Bora na sisi pia kujifunza kutoka kwa
wenzetu.
43. Mheshimiwa Spika, ninayo furaha
kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa baada ya zoezi la muda mrefu la kukusanya
maoni Nchi nzima kuhusu Mpango huu ambapo Waheshimiwa Wabunge nao walishiriki
kutoa maoni yao kuhusu Utawala Bora, sasa hivi Nchi yetu, imefikia hatua muhimu
katika Mchakato huo wa kujitathmini kiutawala bora.
44. Tarehe 26 Januari 2013, Ripoti ya Hali
ya Utawala Bora hapa nchini iliwasilishwa mbele ya Wakuu wa Nchi za APRM Addis
Ababa, Ethiopia ambapo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wetu alipata
fursa ya kuzungumzia mwelekeo wa Nchi yetu katika kujenga Taifa imara zaidi
katika kipindi cha miaka 50 ijayo.
45. Mheshimiwa Spika, katika Ripoti hiyo
ambayo itatumika kama rejea, zimeainishwa
juhudi zetu kubwa za kulinda amani Nchini. Pamoja na kuimarisha Utawala Bora wa
Sheria na Haki za Binadamu. Aidha, kupitia Ripoti hiyo, wenzetu katika masuala
ya kuendesha Utawala Bora, Barani Afrika na Duniani kwa ujumla wametambua
jitihada zetu pamoja na mambo mengine katika kuulinda Muungano, kuimarishwa kwa
mapambano dhidi ya Rushwa na zaidi ya yote wamejua sura ya Tanzania katika
ukombozi na utetezi wa amani Afrika ambao Nchi yetu imepongezwa sana kwa juhudi
zake.
46. Ripoti hiyo pia imeainisha changamoto
ambazo wenzetu wa Afrika wanadhani tunapaswa kuzifanyia kazi zaidi. Changamoto
hizo ni pamoja na suala la kushughulikia Kero za Muungano, kuimarisha zaidi
juhudi za kuondoa umaskini na kuilinda amani ya Nchi yetu hasa kutokana na
chokochoko za Kidini zilizoanza kujitokeza. Tumeaswa kuutumia vyema mchakato wa
sasa wa Mabadiliko ya Katiba kuijenga Tanzania bora zaidi katika miaka 50
ijayo.
47. Mheshimiwa Spika, kuwasilishwa kwa
Ripoti hiyo ya APRM kwa Wakuu wa Nchi wa Mpango huu ndio mwanzo sasa wa
Serikali yetu ya kuimarisha maeneo yaliyoonekana kuwa tunafanya vyema. Pia
hatua hiyo inatoa fursa ya kuanza kutekeleza Mpangokazi wa Miaka Mitano ambao
umeainisha namna gani ya kuyafanyia kazi maeneo ambayo wananchi waliyaona kuwa
yanapaswa kufanyiwa kazi zaidi. Suala hili liliwekewa msisitizo na Mheshimiwa
Rais katika Hotuba yake ya Mwisho wa Mwezi Januari 2013 aliyoitoa kwa Taifa.
48. Mheshimiwa Spika, kutokana na manufaa
ya APRM kama daraja kati ya Serikali na
Wananchi wa kutatua matatizo yetu kwa pamoja, Serikali itaendelea kuiimarisha
Taasisi ya APRM hapa Nchini ili iweze kuwa kitovu chetu cha fikra (think tank)
katika kushauri kuhusu masuala ya Utawala Bora Nchini. Vilevile, kuiwezesha
Taasisi hii kuendelea kuwa kiungo kati ya Serikali yetu na Wananchi wake katika
kutathmini na kutupatia mrejesho juu ya mipango na Sera zetu za maendeleo.
49. Aidha, Serikali itaendelea kufadhili
shughuli za APRM, kuiimarisha Taasisi kwa raslimali watu na fedha kwa ajili ya
kazi pana zaidi za kutoa ushauri, kuunganisha Wadau mbalimbali na kuendelea
kuratibu tathmini nyingine katika siku zijazo kwa lengo la kujipa nafasi ya
kujikosoa ili kujisahihisha. Napenda kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya
Nje, Ulinzi na Usalama wakishirikiana na Sekretariati ya APRM Tanzania kwa kazi
nzuri waliyoifanya ambayo imetuwezesha kufikia mafanikio hayo.
UANZISHAJI WA MAENEO MAPYA YA
UTAWALA
i) Uanzishaji wa Mikoa na Wilaya
50. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge
watakumbuka kuwa, mwezi Machi 2012, Mheshimiwa Rais aliridhia kuanzisha Mikoa
Mipya Minne (4) na Wilaya 19. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba,
Serikali sasa imekamilisha mchakato wa kuanzisha maeneo hayo Mapya ya Utawala,
kwa kuanzisha Mikoa Minne ya Geita, Simiyu, Njombe na Katavi. Aidha,
imekamilisha uanzishwaji wa Wilaya 19 za Buhigwe, Busega, Butiama, Chemba,
Gairo, Ikungi, Itilima, Kakonko, Kalambo, Kaliua, Kyerwa, Mbogwe, Mkalama,
Mlele, Momba, Nyang’wale, Nyasa, Uvinza na Wanging’ombe. Mikoa na Wilaya hizo
tayari zimeshaanza kufanya kazi na kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi.
Vilevile, Mheshimiwa Rais alishafanya Uteuzi wa Viongozi Wakuu wa Mikoa na
Wilaya Mpya. Serikali imeendelea kupeleka Watumishi na kuanza kujenga
miundombinu muhimu katika maeneo husika. Hata hivyo, pamoja na dhamira njema ya
Serikali ya kuanzisha maeneo hayo, bado zipo changamoto nyingi, ikiwemo kupata
Watumishi wa kutosha ambazo Serikali inaendelea kuzitatua.
ii) Uanzishaji wa Halmashauri
51. Mheshimiwa Spika, ili kupeleka huduma
karibu zaidi kwa Wananchi, Serikali pia iliazimia kuanzisha Halmashauri Mpya
37. Uanzishaji wa Halmashauri hizo unaendelea na upo katika hatua mbalimbali
kwa kuzingatia makundi yafuatayo:
Kundi la Kwanza,
linahusu Halmashauri Mpya 8 za Manispaa, Miji na Jiji pamoja na Halmashauri
Moja (1) ya Wilaya ambazo mchakato wa uanzishaji wake tayari umekamilika
Kisheria na zimeanza kufanya kazi. Kundi hili linajumuisha Halmashauri za Jiji
la Arusha, Manispaa ya Ilemela, Manispaa ya Lindi, Halmashauri ya Mji wa
Kahama, Halmashauri ya Mji wa Masasi, Halmashauri ya Mji wa Makambako,
Halmashauri ya Mji wa Geita, Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Halmashauri ya
Wilaya ya Busokelo. Halmashauri hizo tayari zimepata Hati na kupangiwa
Wakurugenzi.
Kundi la Pili, linajumuisha
Halmashauri Kumi (10) ambazo mchakato wa kuzianzisha umekamilika na tayari
zimetangazwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 23 Novemba 2012. Halmashauri
hizo ni Kalambo, Nsimbo, Mlele, Bumbuli, Ushetu, Msalala, Mbogwe, Busega, Momba
na Kyerwa. Halmashauri hizo kwa sasa zinaandaliwa Hati ili zianze.
Kundi la Tatu, ni Halmashauri za
Wilaya Kumi (10) ambazo mchakato wa uhakiki wake umekamilika na Amri za
Uanzishaji zimeshasainiwa na wakati wowote zitatangazwa katika Gazeti la
Serikali. Kundi hili linajumuisha Halmashauri za Wilaya za Buhigwe, Kaliua,
Nyang’hwale, Wanging’ombe, Chemba,
Mkalama, Gairo, Nyasa, Itilima na Kakonko. Aidha, zipo Halmashauri
nyingine Nne (4) katika kundi hili ambazo Amri zake zinakamilishwa na hatimaye
zitasainiwa hivi karibuni. Halmashauri hizo ni Butiama, Tarime, Uvinza na
Ikungi.
Kundi la Nne, linajumuisha
Halmashauri Nne ambazo Mchakato wa uanzishaji wake umekamilika isipokuwa
taratibu za Kisheria haziwezi kuanza kwa sababu baadhi ya Kata katika
Halmashauri hizo ni mpya, hivyo hakuna Madiwani. Halmashauri hizo Nne (4) ni za
Miji ya Kasulu, Handeni, Tunduma na Nzega. Mathalani, katika Halmashauri ya Mji
wa Kasulu kuna Kata 14, na kati ya hizo, Kata 6 ni mpya na hazina Madiwani. Kwa
upande wa Halmashauri ya Mji
wa Handeni ina
jumla ya Kata 12, kati ya hizo 9 ni mpya na hazina Madiwani. Aidha,
Halmashauri ya Mji wa Tunduma ina Kata 5 mpya na zote hazina Madiwani na
Halmashauri ya Mji wa Nzega ina Kata 10, na kati ya hizo Kata 3 ni mpya na
hazina Madiwani.
52. Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha
maeneo hayo mapya ni kuwawezesha Wananchi kupata huduma karibu zaidi kwa
Wananchi. Nitoe wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Watendaji wote kuwaongoza
Wananchi kutumia fursa hiyo ya kuanzishwa kwa maeneo hayo katika kujiletea
maendeleo. Serikali itaendelea kupeleka huduma zaidi karibu na Wananchi ili
kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo hayo. Aidha, Serikali itaweka
utaratibu wa kuzipatia Halmashauri zinazoanzishwa Watumishi hatua kwa hatua.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI
DHIDI YA WATANZANIA WALIOFICHA FEDHA HARAMU NJE YA NCHI
53. Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Novemba,
2012, Bunge lilipitisha Azimio Na. 9/2012 kuhusu kuitaka Serikali kuchukua
hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje ya Nchi kufuatia Hoja
Binafsi iliyowasilishwa na Mheshimiwa Zitto Kabwe (Mb). Azimio hilo linahitaji,
pamoja na mambo mengine, Serikali iwasiliane na Benki ya Dunia kupitia Kitengo
cha Asset Recovery Unit ili mabilioni yanayomilikiwa na Watanzania katika
Mabenki nje ya Nchi ambapo hufichwa kwa kukwepa kulipa kodi yarudishwe na kwamba
Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya Nchi waeleze wamezipataje ili
TAKUKURU wachukue hatua za Kisheria dhidi ya watu wote wenye kumiliki fedha na
mali kinyume na mapato yao halali. Aidha, iliazimiwa na Bunge na Serikali
ikakubali kwamba, katika Mkutano wa Bunge wa 11 italeta Taarifa ya hatua
iliyochukuliwa ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya Nchi.
54. Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Desemba,
2012, Mheshimiwa Rais aliridhia kuundwa kwa Kamati Maalum ya Kitaifa
kushughulia hoja hiyo ya kuitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania
walioficha fedha haramu nje ya Nchi. Kamati hiyo inaundwa na Wajumbe wanane
wanaotoka katika Taasisi za Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu; Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa; Jeshi la Polisi; Benki Kuu ya Tanzania;
Usalama wa Taifa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kazi za Kamati hiyo
ni:
(i) Kuchunguza na kubaini majina ya
Watanzania wanaodaiwa kuficha fedha nje ya Nchi kinyume na Sheria na Kanuni za
Nchi;
(ii) Kuchunguza iwapo fedha hizo ni haramu au
la;
(iii) Kutambua Mabenki na Nchi
zilizofichwa fedha hizo;
(iv) Kuandaa mashtaka dhidi ya Watanzania
watakaobainika kuficha fedha haramu nje ya Nchi; na
(v) Kuishauri Serikali jinsi ya kuzuia
uhalifu wa makosa ya fedha.
55. Mheshimiwa Spika, Kamati hii imeanza
kazi zake rasmi tarehe 9 Januari 2013 kwa kupanga namna ya kutekeleza kazi zake
ikiwemo kukusanya taarifa kuhusu Watanzania wanaodaiwa kutorosha fedha haramu
nje ya Nchi na kuangalia namna ya kupata taarifa muhimu nje ya Nchi. Kamati
hiyo inaratibiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
56. Ili
kuiwezesha Kamati hii kufanya kazi yake kwa ufanisi ni wazi kwamba itahitaji
kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Wananchi kwa kutoa taarifa mbalimbali
kuhusu suala hili. Hivyo, natoa wito kwa Wananchi wote wenye taarifa sahihi na
za ukweli zinazoweza kuisadia Kamati kutekeleza kazi hii wanahimizwa wajitokeze
kutoa maoni yao
kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kushirikiana kwa karibu na
Kamati iliyoundwa na Serikali. Aidha, nawaomba Waheshimiwa Wabunge nao kutoa
ushirikiano wa kufanikisha kazi za Kamati hii.
HITIMISHO
57. Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia
napenda niwashukuru wote waliofanikisha Mkutano huu wa Kumi wa Bunge. Kipekee
nikushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza vizuri ndani ya Bunge
lako Tukufu. Nimshukuru vilevile, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa
kuendesha Vikao vya Bunge kwa ufanisi. Aidha, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge
kwa michango yenu. Nimshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake kwa huduma
nzuri walizozitoa wakati wote tukiwa hapa. Niwashukuru Watendaji wa Serikali na Taasisi mbalimbali kwa
kutekeleza majukumu yao
vizuri ili kufanikisha shughuli za Bunge zilizopangwa. Niwashukuru Waandishi wa
Vyombo vya Habari kwa kutufikishia habari kwa Wananchi yale yaliyojiri hapa
Bungeni na kwa wakati. Vilevile, navishukuru Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa
kazi yao nzuri
na Madereva wote kwa huduma zao kwa Washiriki wa Bunge hili.
58. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema
hayo, naomba niwatakie Safari Njema na sasa natoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu
liahirishwe hadi Siku ya Jumanne tarehe 9 Aprili, 2013 Saa 3:00 Asubuhi kwenye
Ukumbi huu hapa Dodoma.
59. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !